Utafiti: Watanzania wana imani na Awamu ya Sita

DAR: UTAFITI uliofanywa na Taasisi inayojishughulisha na Utafiti, masuala ya Uchumi, Umaskini na Maendeleo ya Nchi ( Repoa), umeonesha Watanzania wana imani na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Mkurugenzi wa Utafiti Repoa, Dk Lucas Katera amesema hayo alipokuwa akiwasilisha repoti ya Mpango wa Tisa wa Afro Barometer.

Amesema katika masuala ya uchumi, Watanzania wanahofia kuhusu kupanda kwa bei za vitu na ajira kwa vijana, lakini wana matumaini na muelekeo kama nchi kutokana na utendaji kazi wa serikali na kwenye baadhi ya mambo.

“Asilimia 61 ya Watanzania wanafurahia utawala na uchumi, lakini pia asilimia 82 wameoneshwa kuridhishwa na masuala ya elimu, huku asilimia 69 wakiridhishwa na huduma za afya zinazotolewa,” amesema Katera.

Katika eneo la utawala na sheria, utafiti unaonesha kuwa asilimia 82 wa Watanzania wametoa maoni yao kuwa Rais anaheshimu Mahakama na Sheria, huku asilimia 81 maoni yaliyokusanywa yanaonesha Rais anaheshimu Mahakama.

Kwa upande wa imani katika taasisi za umma, Dk Katera alisema utafiti umebaini kuwa asilimia 82 raia wana imani na Rais, huku asilimia 78 wakionyesha imani yao kwa Bunge lakini pia asilimia 79 wana imani na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

 

“Asilimia 84 ya Watanzania wana Imani na Chama cha Mapinduzi wakati asilimia 45 wakiamini vyama vya upinzani,” amesema Dk Katera.

Amesema katika mapambano ya kukabiliana na rushwa kiwango kimepanda kwa asilimia 65 tofauti na tafiti iliyopita ya kipindi cha miaka 15 iliyopita.

“Tafiti inaonesha kuwa serikali imejitahidi kupunguza masuala ya uhalifu kwa kufikia asilimia 75, ambapo sasa watu wanaweza kutembea bila hofu, lakini pia asilimia 82 imeridhishwa na serikali kwa kuweka usawa wa kupata nafasi kwa wanawake,” amesema Dk Katera.

“Asilimia 80 wanafuraha jinsi demokrasia inavyofanya kazi nchini Tanzania, asilimia 86 raia wamekiri kuwa huru kuongea lolote wanalofikiria huku asilimia 94 wanaamini kuwa wanaweza kujiunga na chama chochote cha siasa.

“Asilimia 66 raia wamekubali serikali kufunga taasisi yoyote inayoenda tofauti na sera huku asilimia 1 wakiunga mkono kuwa wana haki ya kujiunga na taasisi yoyote ambayo serikali haikubaliani nayo,” amesema Dk Katera.

Amesema kuwa asilimia 55 wametoa maoni kuwa serikali wana haki ya kuzuia vyombo vya habari ambavyo vitachapisha habari itakayoleta taharuki wakati asilimia 49 wakisema vyombo vya habari vina haki ya kuchapa habari au wazo lolote bila kuzuiwa na serikali.

“Asilimia 84 ya Watanzania wana Imani na Chama cha Mapinduzi wakati asilimia 45 wakiamini vyama vya upinzani,” amesema Dk Katera.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button