DAR ES SALAAM: Asilimia 70 ya watanzania wanaishi katika nyumba za kupanga huku wanaojenga wakichukua muda mrefu zaidi ya miaka 18.
Hayo yameelezwa katika ripoti ya utafiti wa ‘Housing Microfinance (HMF)’
uliofanywa na Shirika la Habitat for Humanity International (HFHI) na Tanzania Mortgage Refinance Company (TMRC) iliyozinduliwa Novemba 9, 2023 jijini Dar es Salaam.
Utafiti huo ulifanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Dodoma kwa wananchi wenye umri wa miaka 25 hadi 50 wakiangazia hali ya vipato vyao.
Mkurugenzi wa Nyumba na Fedha kutoka Habitat For Humanity Internation, Daniel Mhina akizungumza amesema watanzania wengi hawana kipato cha kumudu kujenga nyumba na wanaojenga huchukua muda mrefu.
“Unapojenga nyumba muda mrefu kwa miaka 18 gharama zinaongezeka, zinakuwa kubwa kuna kurekebisha mabati, kupaka rangi kwa mtanzania wa kawaida anatakiwa kupata mkopo kwenye huduma za kifedha, changamoto tuliyoiona, huduma za kifedha hazina mikopo inayoendana na matakwa ya watanzania,”amesema Mhina
Utafiti huo umeonyesha kuwa kaya nyingi za kitanzania zinaishi kwa kipato cha chini na cha kati zinazopata kati ya Sh 80,000 ($34) hadi Sh milioni 1.5 ($630) kwa mwezi.
Ripoti hiyo inasema wananchi waliohojiwa walidai kuwa wangependelea kukopa na kila mwezi kurejesha sh 5,000 na wengine walipendekeza rejesho kuwa na ukomo wa sh 80,000.
Hata hivyo ripoti hiyo imeonyesha kuwa changamoto kubwa iliyopo kwa wahitaji wa mikopo ni kutokuwa na uwezo wa kumudu vigezo vinavyohitajika katika taasisi nyingi za kifedha ikiwemo mabenki, unyanyapaa na kutoaminika kwa wajengaji.
Hata hivyo, akizungumzia ripoti hiyo, Mhina anasema uhusiano wa Habitat For Humanity Internatinal na TMRC, wameleta taasisi za kifedha pamoja na kuichambua ripoti hiyo ambayo lengo ni kutoka na majibu ya namna ya kuwakwamua watanzania ili waishi kwenye makazi bora.
“Tutatafuta wadau wawili au watatu ambao tutashirikiana nao ili waweze kutoa mikopo, inawezekana kwenye masoko mengine wenzetu Kenya wameweza, nchi nyingine wameweza lakini Tanzania bado,”amesema na kuongeza
“Tunaweza kuwasaidia watu wakapata makazi bora, kwa mfano tumeweza kutoa mkopo wa sh milioni 190 kwa wananchi 400 ukiangalia kwenye mikopo ya kawaida ya kibenki wanaweza kuwasaidia watu 400 katika nyumba zao za makazi.
“Ni changamoto inayotulazimu kuja na suluhisho kwa wananchi wa kima cha chini na cha kati,”amesema
Amesema kima cha chini cha mikopo hiyo ni sh 100,00 hadi sh milioni 2 ambazo mtu ataweza kukopa kwa ajili ya kufanya marekebisho madogo madogo kwenye nyumba yake na kurudisha ndani ya miezi sita.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa TMRC, Oscar Mgaya amesema waliona ipo haja ya kuanzisha mikopo ya nyumba ndogo kwa watu wa kipato cha chini na cha kati ambao wana tabia ya kujenga nyumba zao hatua kwa hatua kwa kutegemea pesa kidogo wanayopata.
“Mikopo hii itawezesha kuchukua mikopo midogo midogo kwa ajili ya kujenga nyumba zao kwa awamu. Kwa mfano, mtu anaweza kuchukua mkopo kujenga msingi, kisha baada ya kurejesha anaweza kuchukua mkopo mwingine kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo,” amesema.
Kwa upande wa Mwakilishi wa Habitat Tanzania, Fotunata Temu amesema watanzania wemeongezeka kwa mujibu wa sensa ni zaidi ya milioni 60 lakini hakuna makazi bora yenye staha.
Amesema kwa mwaka kuna nakisi karibu nyumba 200,000 kila mwaka, uwezo wa watu kujitengenezea makazi bora ni changamoto, gharama ni kubwa na makazi ni moja ya mahitaji ya binadamu, vipato vya watu ni vidogo.
“Tunaona watu wanavyojenga nyumba kidogo kidogo hata ubora wake unakua sio mzuri ila ndio wafanyaje, ndio maana Habitat tunaingia kusaidia ujenzi wa makazi.