Utafiti: Wengi wasema huduma za jamii zimeboreshwa

TAASISI ya Twaweza imesema asilimia 68 ya wananchi waliohusishwa kwenye utafiti wanasema huduma za jamii katika kipindi cha miezi sita iliyopita, hasa sekta ya elimu zimeboreshwa.

Taasisi hiyo pia imeeleza kuwa asilimia 60 ya waliohojiwa wameeleza kuridhishwa na kuboreshwa uhuru wa kujieleza, uhuru wa kisiasa umeimarika (56%), ulinzi na usalama (59%) na kupungua kwa unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto (61%).

“Kwa ujumla, wananchi wengi wanasema nchi iko kwenye mwelekeo sahihi (30%) na wachache (25%) wanasema nchi haiko kwenye mwelekeo sahihi,” ilieleza taarifa hiyo kwa vyombo vya habari.

Kwa mujibu wa Twaweza, taarifa hiyo ni matokeo ya utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika mara kwa mara kwa njia ya simu za mkononi.

“Takwimu hizi ni za awamu ya saba ya utafiti kwa njia ya simu, ambapo jopo la wahojiwa 3,000 walipigiwa simu kati ya tarehe 18 Juni na 12 Julai 2022,” ilieleza taarifa hiyo.

Ilieleza kuwa maoni ya wananchi kuhusu tozo za miamala ya fedha kwa njia ya simu yanatofautiana, wengi wanakubali kuwa tozo hiyo ni njia muhimu ya serikali kukusanya mapato (67%) na kwamba inasaidia kumfanya kila mtu achangie maendeleo ya taifa (63%).

Taarifa hiyo ilieleza kuwa wananchi wametaja miradi ambayo wangependa inufaike na tozo za miamala ikiwemo huduma za afya (57%), elimu (50%), ujenzi wa barabara (38%), huduma za maji (33%), umeme (20%), kilimo (18%) na mikopo (17%).

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze aliishauri serikali ipanue wigo wa kodi ili kuongeza mapato kugharamia huduma za jamii.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button