Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi amemueleza Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dk Akinwumi Adesina kuwa sekta ya utalii visiwani humo inachangia asilimia 30 ya pato la taifa.
Dk mwingi amezungumza hayo leo Jumamosi Februari 25, 2023 alipoupokea ujumbe wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, ukiongozwa na Rais wake Dk Akinwumi Adesina Ikulu, Zanzibar.
Rais Dk Mwinyi ameishukuru benki hiyo kwa kuunga mkono miradi mbalimbali ya maendeleo Zanzibar ikiwemo ya kijamii katika sekta ya Afya , barabara, maji na sekta ya usafiri.
Dk Adesina alimuelezea mwenyeji wake Rais Dk Mwinyi miradi ambayo Benki hiyo inasaidia zaidi ujenzi wa barabara na sekta nzima ya usafiri.
Alisema kwa sasa benki yake inasaidia ujenzi unaoendelea wa barabara ya Bububu-Mahonda-Mkototoni, ujenzi wa barabara Tunguu-Makunduchi na ya Mkoani- ChakeChake.
Alisema benki hiyo imejikita kusaidia ujenzi wa uwanja wa ndege mpya wa Pemba na miradi kadha ikiwemo ya maji na ujenzi wa masoko.
Ameongeza kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika imetenga Dola milioni 15 kuunga mkono sekta zilizochini ya Uchumi wa Buluu.