Utani Simba, Yanga zamani ilikuwa raha sana

Yanga iliitwa Kuala Lumpur, Kandambili,Simba iliitwa Sunderland, Abidjan

MIAMBA ya soka nchini Simba na Yanga inaumana leo jioni Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2022/2023, ukiwa ni mchezo wa marudiano.

Nami naweka makala maalumu kuzungumzia kuhusiana na mechi baina ya miamba hiyo zilivyokuwa miaka ya nyuma, iliyoandikwa na mwandishi nguli nchini Salim Said Salim. Twende sote.

Mwishoni mwa mwaka 1965 nilihamishwa kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam  na kujiunga rasmi kama mfanyakazi wa kuajiriwa na magazeti ya kampuni ya Tanganyika Standard (sasa Daily News).

Siku moja nilipofika ofisini, Barabara ya Maktaba, kutoka Magomeni Mikumi na kuweka vespa yangu pembeni niligundua kuwepo gari ya makachero (CID) ambayo nilikuwa nikiona sana mahakama  ya Kivukoni.

Fikra zangu zilifanya kudhani palitokea wizi wa magazeti na ndio maana wakawepo makachero. Polepole nilielekea ofisini na huko nikakuta waandishi na wahariri wanadadisiwa na makachero.Nilipomuuliza tarishi wa ofisi, mzee Shaabani, kulikuwa na nini, alinijibu : ” Wewe hujasoma Sunday News”?

Aliniambia habari za Nyerere kufikishwa mahakamani zimeleta kizazaa. Haraka haraka nililitafuta gazeti na kukuta habari iliyokuwa na kichwa cha maneno: “Nyerere in court”, yaani Nyerere mahakamani.

Kichwa hiki cha habari kiliwaudhi wakubwa kwa vile yeyote aliyeisoma aliamini  Baba wa Taifa, Rais  Nyerere amefikishwa mahakamani.

Ni kweli Nyerere alifikishwa mahakamani siku ya Jumamosi, lakini alikuwa  hayati Joseph Nyerere, mdogo wa Mwalimu. Lakini ili kuuza gazeti kilitafutwa kichwa cha habari cha kuvutia na ikawa balaa.

Siku hizi vichwa vya habari vya aina hivi vimekuwa vya kawaida. Leo utasikia Waziri kafumaniwa na ukisoma utakuta kijana ambaye jina lake ni Waziri ndiye aliyekamatwa ugoni.

Wakati makachero wakiendelea na udadisi wao niliteremka ngazi na kuondoka na vespa yangu kuelekea Kariakoo bila ya kufahamu nini hasa kilichonipeleka huko.

Nilipofika Kariakoo nilimtembelea mzee wetu, marehemu Mangara Tabu Mangara, Mwenyekiti wa Yanga, ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa waandishi wa habari. Mimi binafsi nilielewana naye sana.

Nilienda nyumbani kwake, nyuma ya soko kuu la Kariakoo na kuwakuta vijana watatu, wote wachezaji mpira. Mmoja wao alikuwa Abrahman Lukongo, mshambuliaji hatari wa Yanga na timu ya taifa wakati ule.

Walikuwa wanaagana na mzee Mangara aliyekuwa amekaa barazani akiwa amevaa msuli. Nakumbuka mzee Mangara aliwaambia: ” Mzaha wenu mnapokutana na Sanda (zamani Sunderland na leo Simba) mnatuponza sisi. Hawa sio watu wa kutufunga”.

Walipoondoka nilisalimiana na mzee Mangara. Nikampa pole kwa kufungwa na Sunderland siku iliyopita katika mchezo wa kirafiki.

Mzee Mangara aliniuliza kama nilikwenda kumsalimu au kumtania. Nilimjibu: ” Yote mawili”.

Alicheka sana na kuniuliza habari za wazee na marafiki zangu. Mara nikasikia gari likipiga honi mfululizo kwa nguvu na nilipoangalia niliiona ile Peugeot 304 iliyokuwa maarufu jijini wakati ule, gari la jirani yangu Magomeni Mikumi, mzee Habib. Huyu alikuwa kiongozi  maarufu wa klabu ya Sunderland.

Mzee huyu hata Sunderland ilipobadilishwa jina aliendelea kusema klabu yake ni Sunderland na sio Simba. Mzee Habibu pia alijulikana kwa lile jina la pili la Sunderland, yaani Abidjan.

Lakini zaidi mwenyewe akipenda kuitwa ” Under line”, yani chini ya mstari. Hii ilitokana na yeye kupenda wachezaji wa pembeni walioukimbiza mpira kwa
kasi kuelekea kwenye kibendera cha kona, kama marehemu Khamis Mtoto na marehemu Salim Ali Jinni na baadaye marehemu Willy Mwaijibe wa Simba.

Wakati Sunderland ilipokuwa inaitwa Abidjan nayo Yanga ilikuwa na majina mawili, Kuala Lumpur na Kanda Mbili, yaani klabu ya makabwela.

Hapo tena mzee Mangara akasema: “Haya tena…shetani huyo kafika, laa ..haula”.

Mzee Habibu akateremka kwa mbwembwe akiwa na mkoba uliokuwa na machungwa, akasalimiana na mzee Mangara na kutaniana kidogo na akaitwa mtoto kupokea mkoba wa machungwa.

Mzee Habibu akamtambia sana mzee Mangara kwa kumwambia; ” Mtoto wacha kupiga mayowe…wache watu waone wenyewe”, na kumwambia :”Mimi ni mkubwa kwako”.

” Wazee wako walijua kuwa utapata tabu kwa Sanda na ndio maana wakakupa jina la Tabu Mangara na nataka ujuwe hutang’ara mbele yangu”, mzee Habibu aliongeza.

Akapita muuza kahawa na kashata na mzee Habibu akanunua birika zima na mkoba wa kashata na kumwambia mzee Mangara kuwa hiyo ni zawadi ya Sunderland kwa watoto wao wa Yanga.

Mzee Mangara alibaki kucheka na kusema : ” Ama kweli Mswahili akipata..makalio hulia mbwata”.

Akaitwa mtoto mdogo aliyekuwa ndani kuja kupokea zawadi aliyoleta mzee Habibu, lakini mzee Mangara alionekana kuwa na wasiwasi na ile zawadi. Yule mtoto alipokuja kupokea mkoba mzee Mangara alimwambia:” Mwambie bibi ampikie chai mzee Habibu…maana kwake kafukuzwa na hakunywa chai.

Wakati huo kila aliyepita pale barazani walipokaa wazee hawa wawili alikaribishwa kahawa na kashata.

Haikupita muda akaja tena yule mtoto, akiwa na mkoba mkono mmoja na mpira wa kuchezea tenisi (chandimu), ameushika mkono wa pili na kusema kuwa ulikuwemo ndani ya mkoba.

Mzee Mangara alimuangalia rafiki yake na kumwambia: ” Nilijua mimi …ule mkoba ulikuwa na mambo yako”.

Naye mzee Habibu akamwambia mtoto kile chandimu ni mpira wa babu kwa sababu Yanga walikuwa kama watoto… bora wacheze chandimu. Alimwambia yule
mtoto ampe babu yake kile chandimu na machungwa ni yao wao.  Mzee Mangara akapokea kile kipira na kusema: ” Ahsante…lakini na wewe unayo siku yako.”

Walicheka na kufurahi.Wakaulizana habari za familia, huku wakitaniana. Nilikaa nao kwa muda na kuwaacha barazani. Baadaye nilipata habari kwamba mzee Habibu alimchukua swahiba wake, mzee Mangara nyumbani kwa chakula cha mchana.

Niliporudi ofisini nilikuta aliyekuwa Mhariri wa gazeti la Sunday News, Thomson (masharubu) amepewa saa 24 kuondoka nchini kwa kubuni kile kichwa cha maneno cha Nyerere mahakamani.

Lakini mbali ya somo la umuhimu kwa chombo cha habari kufuata maadili nilipata siku ile juu ya maelewano ya wanamichezo wazee ambao walikataa kandanda kuwagawa na kuleta uhasama, bali walitumia tafauti zao za mapenzi ya klabu hizi mbili kongwe kuzidisha urafiki wao wa utotoni.

Hii ilikuwa taswira ya michezo nje ya kiwanja ambayo siwezi kuisahau, abadan. Siku hizi mashabiki wakitaniana kidogo tu utasikia wanatukanana au kuingiana maungoni kwa kuchapana masumbwi na hata kuchinjana visu.

Leo hii Watanzania tujiulize viongozi wangapi wa klabu zinazojiita mahasimu wanatembeleana nyumbani, kutaniana na kufurahi pamoja?

Wengi huenda nyumba za viongozi wenzao panapotokea msiba wa mmoja wao kuiaga dunia na mara nyingi huwa ni kwa mara ya kwanza na ya mwisho.

Kwangu mimi utani wa wazee hawa wawili ambao wote sasa ni marehemu ni moja ya fundisho ambalo wazee wa zamani wa Yanga na Simba waliwaachia waliowafuatia.

Siku hizi baadhi ya viongozi huoni kuheshimiwa na badala yake watu wanakashifiana na kutukanana.

Wakati mzee Habibu aliyekuwa dereva wa teksi akienda uwanjani pale Sunderland ilipocheza, mzee Mangara aliyekuwa mpiga chapa mkuu wa serikali alifuatilia
matokeo redioni.

Habari Zifananazo

Back to top button