UPANDE wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi namba mbili, 2022 inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya na wenzake wanne wameomba shauri hilo kuhamia mahakama kuu ili kesi hiyo ianze kusikilizwa na washtakiwa wajue hatma yao.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Salome Mshasha, wakili wa utetezi, Hellen Mahuna, aliiomba mahakama kulihamisha shauri hilo mahakama ya juu kwani mahakama ya sasa haina uwezo wa kuisikiliza kesi hiyo.
Alisema kuhamishwa kwa maelezo, vielelezo, ushahidi na masuala mengine, kutaipa mahakama kuu uwezo kuendeleza shauri hilo ikiwa ni baada ya kuchukua muda mrefu katika Mahakama ya Hakimu mkazi Moshi ambayo haijapata kibali cha kusikiliza kesi hiyo.
“Tumetoa hoja zetu mara kadhaa lakini bado upande wa Jamhuri umeendelea kudai upelelezi haujakamilika licha ya awali Juni mosi, 2022 walidai upelelezi umekamilika…tufanye ‘Committal Proceedings’ shauri hili lihamie mahakama kuu,” alisema.
“Ni rai yetu sisi kama utetezi, tuombe upande wa Jamhuri kuharakisha upatikanaji wa kibali kutoka kwa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka (DPP) kutoa kibali cha kusikiliza kesi hii lakini pia Jamhuri ikamilishe upelelezi ili washtakiwa wajue hatma yao,” alisema.
Wakili Hellen aliieleza mahakama hiyo kwamba washtakiwa katika kesi hiyo, hususani mshtakiwa wa kwanza Sabaya ambaye anaumwa, wanaendelea kuteseka gerezani bila kujua hatma yao.
Akitupilia mbali hoja ya utetezi iliyotolewa Agosti 12, 2022 kutaka mahakama itazame kifungu cha 62 cha tafsiri ya sheria kuwa endapo sheria haijatoa ukomo wa jambo kufanyika, jambo hilo lifanyike kwa uzoefu, hakimu Mshasha alisema hoja hiyo haina msingi.
Alisema kifungu hicho hakiwezi kutumika katika kesi ya uhujumu uchumi lakini pia mahakama haina mamlaka ya kumuamuru DPP kutoa kibali cha kusikiliza kesi hiyo bali jambo hilo litafanyika baada ya ofisi hiyo kujiridhisha na kile inachopanga.
“Mahakama itaendelea kusubiri upelelezi wa shauri hili ukamilike lakini DPP atoe kibali kesi ianzwe kusikilizwa, kinyume na hapo hakuna kitu kitakachoweza kufanyika, kesi hii naiahirisha hadi Septemba 12 mwaka huu, itakapotajwa tena,” alisema.
Hata hivyo, hakimu Mshasha alisema ukiacha hoja za kisheria lakini upande wa Jamhuri katika kesi hiyo kuzingatia hoja za utetezi kwamba shauri hilo limechukua muda mrefu na sasa wakamilishe upelelezi wao.
“Mahakama ni chombo cha kutoa haki, tunataka wananchi wawe na imani na chombo hiki, hili shauri limechukua muda mrefu na sababu ni hiyo hiyo kuwa upelelezi haujakamilika na DPP hajatoa kibali, hebu kamilisheni hili kesi isikilizwe,” alisema.
Akijibu hoja za utetezi, wakili wa serikali, Sabitina Mcharo alisema wamesikia hoja hizo pamoja na rai ya mahakama na kwamba watafanyia kazi jambo hilo ili upelelezi ukamilike na kesi ianze kusikilizwa.