Utoaji mimba holela unaharibu figo

UTOAJI mimba holela unaweza kusababisha matatizo ya figo, wanasema wataalam wa afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa  wa Mwanza, Sekou Toure.

“Ni kwa sababu utoaji huo unatafsiriwa kuwa wa kienyeji, unafanyika vichochoroni pasipo na wataalam wa masuala ya uzazi kusimamia mchakato kutokana na sheria za nchi kutoruhusu utoaji mimba,” wamesema wataalam na kuongeza:

“Matokeo yake baada ya mimba kuharibiwa, mhusika  anaweza kutokwa damu nyingi, lakini isiyoonekana kwa macho, kwani inakimbilia na kujificha katika mfuko wa uzazi na hivyo kuathiri figo.

“Haya ni matatizo yanayoweza pia kumkumba mjamzito baada ya kujifungua,” amesema mtaalam wa figo katika hospitali hiyo, Dk Ezekiel Petro.

Amefafanua kwamba damu ikitoka nyingi na kukimbilia kwenye mfuko wa uzazi maana yake figo inakosa damu ya kutosha kwa ajili ya kazi yake ya kuchuja taka mwili na kuzitoa nje.

Amefafanua zaidi kwamba ndio maana mjamzito anayejifungulia hospitali haruhusiwi wakati huohuo kutoka, ili kutoa mwanya kwa wataalam kuchunguza kama mfuko wake wa uzazi hauhifadhi damu kinyemela.

Ameongeza kwamba kawaida, figo inapokea zaidi ya asilimia 20 ya damu inayosukumwa na moyo kwa kila zamu (ya msukumo).

“Kiasi kinachohitajika kisipotimia, figo itatoa taarifa kwa moyo, na moyo ukisukuma zaidi ya mara tatu bila kiasi kukamilika, ufanyaji kazi wake (figo) utadorora (zitaanza kufeli) na pengine kuharibika kabisa endapo hatua stahiki hazitachukuliwa kwa wakati.

“Na hatua stahiki ni moja tu, ya kusafisha damu ili uchafu utoke nje, ule ambao tayari umezalishwa, lakini ukashindwa kuchujwa na figo kutokana na (figo) kukosa damu ya kutosha kufanya kazi hiyo,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button