Utoaji mimba janga lisilosemwa, linalouwa kimya kimya

ASIA Patrick binti wa miaka 19 amekumbwa na madhila ya kutolewa kizazi na kukatwa miguu yote miwili na vidole tisa vya mikono yake baada ya mimba kuharibika na kukosa fedha shilingi 150,000, ili aweze kusafishwa.

Kuchelewa kupewa huduma ya kusafishwa mimba ambayo imeharibika kulisababisha Asia kupata maambukizi kwenye kizazi ‘Sepsis’ na kufanya atolewe kizazi akiwa binti mdogo, na maambukizi hayo yalipelekea pia kupata ‘Cellulitis’, ambapo seli za mwili zilikufa baada ya mishipa ya damu kuziba.

Huyo ni Asia mmoja, je Asia wangapi wapo mitaani ambao wameacha majeraha makubwa kwenye maisha yao au kupoteza maisha?

Advertisement

Sheria na sera ya utoaji mimba nchini Tanzania ina utata na inachanganya. Sheria ya makosa ya jinai huidhinisha utoaji mimba, ili kuokoa maisha ya mwanamke, lakini haijaweka wazi kama utaratibu huu utalinda afya ya mwili na akili ya mwanamke.

Hofu ya kushtakiwa, ambayo ipo kwa wanawake na watoa huduma ya afya pia, husababisha wanawake watoe mimba kwa siri kwa njia ambazo mara nyingi huwa si salama.

Tanzania ni kati ya nchi zenye uwiano wa juu wa vifo vya wajawazito duniani 410 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa wakiwa hai, na utoaji mimba usio salama ni moja kati ya sababu zinazoongoza.

Utoaji mimba usio salama unachangia zaidi ya theluthi moja ya wanaolazwa hospitalini kutokana na matatizo yanayohusiana na mimba na takribani robo ya vifo vya uzazi.

Serikali inatumia Sh bilioni 10.4 kwa mwaka kwa ajili ya kugharimia matibabu kwa wanawake walioharibikiwa au kuharibu mimba (PAC).

Hiyo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Guttmacher ya Marekani kwa kushirikiana na watafiti wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas).

Fedha hizo zilitumika mwaka 2018 kuwahudumia wanawake 77,814 waliopatiwa matibabu hayo, ili kunusuru maisha yao baada ya kuharibikiwa au kuharibu mimba, huku wengine 114,272 wenye uhitaji wa matibabu hayo wakiyakosa kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa mujibu wa utafiti huo, fedha hizo zilitumika kwa sababu baadhi ya waathirika walishindwa kumudu gharama za matibabu, huduma za matibabu baada ya kuharibika mimba kutopatikana katika maeneo yote, hasa vijijini, hofu ya kubainika amebeba ujauzito na mtazamo hasi wa jamii dhidi ya huduma hizo.

Kiwango cha kitaifa cha utoaji mimba nchini ni wanawake 36 kwa kila wanawake 1,000 walio kwenye umri wa uzazi wa kati ya miaka 15 hadi 49.

Utafiti huo unaeleza kuwa, kiasi hicho cha fedha kinaweza kufikia Sh bilioni 25.7 kwa mwaka endapo matibabu hayo yatawafikia wanawake wote wenye uhitaji.

Watafiti hao waligundua kuwa, utoaji mimba kwa siri hutokea mara nyingi na huchangia kwa kiasi kikubwa kwenye vifo na kuumia kwa wajawazito.

Mhadhiri wa Muhas, Dk George Ruhago anasema kukabiliana na gharama hizo ni muhimu kama nguvu kubwa ikiwekezwa kwenye elimu na huduma za uzazi wa mpango ili kuepusha mimba zisizotarajiwa.

“Utoaji wa mimba hauruhusiwi kisheria isipokuwa pale inapolazimika kuokoa uhai wa mama, lakini ukweli ni kwamba utoaji mimba upo na kutokana na vitendo hivi kufanyika kwa siri wengi huishia kwenye utoaji mimba usio salama,” anasema Dk Ruhago.

“Wengi huishia kujaribu njia mbalimbali za kutoa mimba na pale wanaposhindwa kutekeleza azma yao na kuwa katika hatari ya kupoteza maisha ndipo hukimbilia hospitali kwa ajili ya kupata msaada wa matibabu.”

Dk Ruhago anasema hali hiyo inathibitisha kuwa inahitajika nguvu kubwa katika elimu ya kujiepusha na mimba zisizotarajiwa, ili kupunguza idadi ya mimba zinazoharibiwa na madhara yanayoambatana na vitendo hivyo.

NINI KIFANYIKE?

Wataalamu wa masuala ya afya ya uzazi wamependekeza kuimarisha juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa huduma, baada ya kuharibika kwa mimba, ambayo kwa sasa inapatikana bila ulinganifu katika maeneo mbalimbali.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na Mhadhiri kutoka Muhas, Ali Said anasema, huduma hizo kuwafikia wahitaji wengi ni muhimu kwa vituo vya afya katika ngazi zote viwe na dawa muhimu za kutosha.

“Vifaa vya kutolea huduma za msingi za baada ya kuharibika kwa mimba, na watoa huduma wa kawaida wanapaswa wapewe mafunzo ya kutoa huduma hizo.

“Ni muhimu kufanyika uwekezaji katika kufanya huduma baada ya kuharibika kwa mimba ili ipatikane katika ngazi zote za mfumo wa afya,” anasema.

Kupunguza utoaji mimba usio salama na vifo vya wajawazito na majeraha yanayohusishwa na utoaji mimba, utahitaji kupanua upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango, ili kuzuia mimba zisizotarajiwa, na kupanua upatikanaji wa huduma za baada ya kuharibika kwa mimba.

Kwa upande wake Dk George Alcard anasema umuhimu wa kujumuisha utoaji wa huduma za uzazi wa mpango kama sehemu ya huduma baada ya kuharibika kwa mimba na kwamba kila mwanamke anayetibiwa kutokana na matatizo yanayohusiana na kutoka kwa mimba apewe ushauri wa kina na nyenzo za uzazi wa mpango.

Kuhusu kuzuia mimba zisizotarajiwa daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake Living Colman, anasema njia za uzazi wa mpango zinaweza kuwa suluhu za mimba zisizotarajiwa.

Baadhi ya njia hizo ni matumizi ya vidonge, sindano na vipandikizi vya kuzuia ujauzito. Kitaalam dawa na vizuizi hivi vinazuia mayai kuzalishwa, hivyo kufanya mimba isitungwe.

“Serikali inaweza kuwekeza katika utoaji wa elimu ya uzazi wa mpango, watu wakafundishwa kwa kina kuhusu njia hizi na namna ya kuzitumia ili kila mmoja aamue kufanya uchaguzi wa njia ambayo itamuepusha kupata mimba isiyotarajiwa,” anasema Dk Colman.

SHERIA:
Mwanasheria Baraka Thomas anasema Sheria ya Tanzania inakataza utoaji mimba kwa namna yoyote isipokuwa tu kama uhai wa mama upo hatarini, haijalishi kama afya ya mama ipo hatarini.

Sheria hizi zinakinzana kiasi na makubaliano kadhaa ya kimataifa kama vile UN International Conference on Population and Development – Cairo, Mkutano wa nne wa dunia wa kinamama huko Beijing, mmoja wa viongozi  alikuwa  Mama Getrude Mongella wa Tanzania (World Conference on Women in Beijing)  Azimio la haki za binadamu (The Universal Declaration of Human Rights (ibara za 1 & 3 &12 &19 & 27.1 na Maputo Protocol kifungu cha 14 (2).

Anasema ni vema sasa, serikali iangalie namna ya kurekebisha sheria za utoaji mimba kuepusha changamoto nyingi za kijamii ikiwemo kutelekeza watoto, changamoto za kiuchumi, kielimu na hasa ki-afya.

“Tumeona pamoja na sheria kukataza, lakini vitendo hivyo hufanyika sana. Na kwa sababu ya kikwazo cha sheria, vitendo hivi hufanywa kwa siri na katika mazingira hatarishi.” Anasema Thomas na kuongeza

“Sheria iangaliwe upya kuwasaidia wakidada. Wapo wanaopata mimba kwa kubakwa au kulaghaiwa kwa kuombwa rushwa ya ngono na maboss, na wengine kwa sababu ya ujinga wa elimu ya uzazi, shida ni kwa wanawake.

Amesema serikali imekuwa ikiboresha huduma za uzazi na uzazi wa mpango, elimu ya uzazi na hata huduma kwa mimba zilizotoka/tolewa (post abortion care) lakini bado haitoshi.

“Nguvu zaidi inahitajika na endapo sheria itarekebishwa maana yake vitendo hivyo vitafanyika katika mazingira salama tofauti na sasa,” amesema.

WHO VIFO VYA UTOAJI MIMBA VINAZUILIKA:

Kaimu Mkurugenzi wa masuala ya afya ya uzazi na utafiti, kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Craig Lissner, anasema takriban kila kifo na majeraha yanayotokana na utoaji mimba usio salama yanaweza kuzuilika kabisa.

 Ndiyo maana tunapendekeza wanawake na wasichana wanaweza kupata huduma za utoaji mimba na uzazi wa mpango wanapozihitaji,” anasema Craig

Kwa mujibu wa WHO ushahidi unaonesha kuwa kuzuia upatikanaji wa huduma za utoaji mimba hakupunguzi idadi ya utoaji mimba unaofanyika.

Amesema vikwazo vina uwezekano mkubwa wa kuwasukuma wanawake na wasichana kutumbukia katika taratibu zisizo salama.

Katika nchi ambako utoaji mimba umewekewa vikwazo zaidi, ni utoaji mimba 1 tu kati ya 4 ambao ni salama, ikilinganishwa na karibu utoaji mimba 9 kati ya 10 katika nchi ambako utaratibu huo umehalalishwa.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *