UTAMADUNI wa kifo unaosababisha watoto ambao hawajazaliwa kuuawa kupitia utoaji mimba japo hufanyika kwa siri na hakuna takwimu zake, unaelekea kuwa kawaida katika jamii licha ya madhara yake kijamii, kiuchumi, kiafya na kiroho. MWANDISHI JOSEPH SABINUS anatumia vyanzo mbalimbali kuonesha madhara ya ukatili huu kijamii.
Fuatilia…
“Inauma kuona mwanamke mwenzangu anaua mtoto wake akiwa bado tumbomi kisha anauweka mwili kwenye mfuko na kumpeleka dampo na wakati mwingine, unasikia eti mbwa wameokota binadamu huyo… Kwa kweli huu ni udhalilishaji wa utu, ukiukaji wa haki ya mtu kuishi na ukatili wa kupindua ambao ni kosa kubwa mbele ya Mungu na mbele ya sheria za nchi.”
Ndivyo anavyosema Jawa Bantulaki, mkazi wa Kongowe Kibaha mkoani Pwani akipinga aina, sababu na visingizio vyote vinavyotolewa kuhalalisha mauaji yoyote yakiwamo ya watoto kwa utoaji mimba.
Anasema: “Kwa kuwa utoaji mimba ni haramu, watu wanatumia njia hatari kiafya zikiwamo nyingine za kienyeji zinazowaweka katika hatari ya kupata madhara mengine ya kimwili na kiakili… Mauaji haya ya watoto huathiri uhusiano kati ya mume na mke na hupunguza upendo katika familia kwani hakuna mwanaume anayependa kuoa mwanamke ambaye amekuwa na historia ya kuua watoto wake mwenyewe kwa kutoa mimba…”
Uchunguzi wa HabariLEO kupitia watu mbalimbali umebaini kuwa, wakati mwingine wazazi, ndugu au mume hushawishi na kulazimisha mwanamke kutoa mimba ingawa baadaye, humbeza.
“Kadhalika, wapo wanawake wakiwamo wasichana wanaokosa uadilifu katika maisha yao na kujikuta katika mimba kabla au nje ya ndoa hivyo, kukengeuka zaidi kwa kutumia mauaji ya utoaji mimba kujaribu kuficha uhalifu wao. Wengine, wameumbuka kwa kupoteza maisha yao na watoto waliotaka kuwaua.”
Mkazi wa Nyantira, Kata ya Kitunda wilayani Ilala, Anita Joachimu anasema: “Utoaji mimba ni aibu na ni kosa kwa sababu familia inaingia katika msiba ambao mwanafamilia ndiye ameua mtu na utoaji mimba unafanya familia kuwa katika maombolezo ya siri na msiba wa mwanafamilia usio rasmi huku wanafamilia wengine wakiwa hawajui kuwa familia yao inaomboleza…”
Anaongeza: “Familia ndilo chimbuko la watu na taifa. Familia inapotindikiwa na wanafamilia, ndivyo hivyo taifa linavyokosa watu. Familia inapokabiliwa na majeraha yanayojiegemeza katika ukatili wa kuua wanafamilia ambao hawajazaliwa, ndivyo hivyo moyo wa ukatili unavyodhihirika katika jamii.”
Stelius Sane, mkazi wa Buza, Dar es Salaam ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari anasema: “Leo tusishangae tunaposikia mama mzazi amemweka mtoto wake mchanga katika mfuko wa rambo na kumtupa vichochoroni au barabarani au kwenye dampo la takataka baada ya kumuua, au tunaposikia baba amemwadhibu mtoto wake kiasi cha kumjeruhi au tunaposikia mama amemchoma mtoto wake moto kwa sababu ya kuiba Sh 500 au eti mtoto amezurura. Hayo ni matokeo ya roho ya ukatili inayojengwa katika jamii kupitia utoaji mimba.”
Sane anaongeza: “Hii ndio laana inayozikabili familia nyingi leo. Tunatupiana lawama juu ya kuporomoka maadili yanayoathiri malezi ya watoto wetu, kama vile hatujui kuwa hiyo inatokana na laana ya kuua watoto wetu ambao hawajazaliwa.”
Mhitimu wa Shahada ya Uzamili ya Ustawi wa Jamii katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW) iliyopo Dar es Salaam, Safari Kitamogwa, anasema: “Ukiona watu wameharibikiwa kimaadili yaani mauaji, ufisadi, ukatili usioelezeka, na matukio mengine ya ajabu, kama vile uporaji, umwagaji damu unaotokana na matumizi ya silaha za moto, ujue hali hiyo inaakisi laana kubwa iliyoikumba jamii hiyo.”
Kuhusu laana na madhara ya mauaji ya utoaji mimba katika familia, chapisho la shirika la kimataifa la kutetea uhai la Human Life International (HLI) linasema: “Babu na bibi wanakata tamaa, hawaoni wajukuu wa kuwapokea na kucheza nao. Shangazi anakosa wapwa, hakuna wa kutaniana naye. Katika Afrika, faraja ya wazee ni kuona kizazi kinarithishwa kwa njia ya wajukuu. Uzao wa watoto ndio ‘bima’ pekee na ya kuaminika katika maisha ya uzeeni.”
“Sasa, kupitia utoaji mimba, si tu kwamba babu na bibi wanakosa wajukuu wa kucheza na kufurahi nao, utoaji mimba unamaliza kizazi na ukoo. Hali hii ni kinyume kabisa cha shabaha ya uumbaji, ndoa na familia. Wanafamilia wanapojihusisha na kusitisha uzao, si tu kwamba wanajimaliza wenyewe, bali wanajifuta katika sura ya dunia.”
Mmoja wa watetezi wa uhai, Magreth Daniel (si jina halisi) wa Buhemba Tarime, anasema wimbi la utoaji mimba linaposhamiri, familia zinawaleta duniani watoto waliopondeka moyo na kujeruhiwa kiakili wakiwamo walionusurika.
Anasema katika hali hiyo, familia zinashuhudia kuzuka kwa vijana katili na wenye vurugu na hasira wanapochokozwa.
“Huu ni ukatili wa wazazi unaopelekwa kwa watoto wao kwa sababu ya mauaji yanayofanyika katika familia. Watoto wanarithishwa tabia ya mauaji kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Katika hali ya kawaida, tunashuhudia vitendo vya ukatili hata kwa makosa madogomadogo. Ukatili wa mama kwa mtoto, baba kwa mtoto, mume kwa mke, mke kwa mume na hata mtoto kwa wazazi wake…,” anasema.
Magreth anayejitambulisha kama mama wa watoto watatu, anasema: “Hapa kunakuwapo mzunguko usiokwisha wa ukatili na mauaji. Familia zinashuhudia kujengeka tabia ya kuwanyanyasa na kuwatelekeza watoto na ndipo tunapopata watoto wanaoitwa wa ‘mitaani’ au wengine wanapenda kuwaita watoto hawa ‘wanaoishi katika mazingira magumu.”
Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (Prolife) Tanzania, Emil Hagamu, anasema utoaji mimba unapofanyika katika familia, laana hurithishwa kwa vizazi vinavyofuatia hadi vizazi vinne. Hii ina maanisha kuwa, ukatili wa mama mmoja utarithishwa kwa watoto, wajukuu, vilembwe na vilembekweza wake.
“Matokeo yake, tunapata mfululizo wa kizazi cha watu si tu katili, bali kisichokuwa na huruma, cha mauaji, cha watu wasio na upendo na kizazi cha watu wasiojali maisha yao wala ya wengine.”
“Hiki ni kizazi cha hovyo kinachofurahia mauaji badala ya uhai. … Katika familia nyingine imekuwa ni fasheni kuua watoto wao wasiozaliwa,” anasema na kuongeza: “ndio maana hata katika masuala ya kiafya, juhudi zifanyike kuokoa mama na mtoto na si kuokoa mama kwa gharama ya mtoto.”
Hagamu ambaye pia ni Mkurugenzi wa HLI, Kanda ya Afrika kwa nchi zinazozugumza Kiingerza anaongeza: “Mama mzazi atamhimiza binti yake kuua mjukuu wake, eti ili binti yake ahitimu masomo na usishangae mume akampatia mkewe fedha za kuua mtoto wao eti kwa sababu anaogopa aibu ya kuzaa katika kipindi kifupi.”
Anasema laana nyingine zinazojitokeza mara nyingi hazina maelezo ya wazi. Anatoa mfano wa mafarakano kati ya mume na mke au vurugu katika maisha ya wanafamilia.
“Hapo inazaliwa hali ya kutoaminiana, kuogopana, kuhisiana vibaya na kwa ujumla wake kunakuwa na kuvunjika si tu upendo wa kindoa, bali pia upendo wa kifamilia,” anasema Hagamu.
Kuhusu matokeo ya hali hiyo katika miundo ya jamii, anasema: “Nani atashangaa leo tunapoona watu wanafurahia matukio ya vifo; na hata kushabikia methali ya Kiswahili isemayo, ‘kufa kufaana!’ … Mauaji yanaposhamiri katika jamii, watu wanakosa huruma hata katika matukio ya vifo na hivyo, kufanya kifo cha mtu kuwa furaha kwa wanaobaki ndio maana tunashuhudia baadhi ya watu wakifurahia ajali ili kupora mali ya majeruhi au wafu.”
“Matukio ya misiba hayaleti tena taswira ya uchungu na maombolezo, bali yamegeuka kuwa shehere za kula na kunywa, na hata kugawana mali za marehemu kabla hata hajazikwa… Katika misiba zitaundwa kamati za mapambo, chakula, sare zitashonwa na wengine watafika kwa wingi si kuomboleza, bali kusherehekea.”
Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Watetezi wa Uhai na Familia (JOLIFA) Tanzania, Frida Manga, anasema kushamiri utoaji mimba kunachangia kufanya watu kukosa huruma hata kwa watu wenye ulemavu na hivyo, kutotimiza jukumu la kuwalinda na kuwasaidia watu wasiojiweza wakiwamo wenye ulemavu.
Mtakatifu Theresia wa Calcutta, aliwahi kusema: “Iwapo mama anaweza kumwua mwanaye wa tumboni, je, kitazuia nini sisi kwa sisi kuuana?”
Hagamu anasema: “Tukiwa na tabia ya kuwaua watoto kabla ya kuzaliwa ni rahisi kuana sisi kwa sisi kwa visingizio vyovyote vikiwamo vya tofauti za kisiasa, kiimani, kiuchumi kati ya maskini na matajiri au hata tofauti za rangi.”
“… Katika imani ya dini zote, utoaji mimba unahesabika kuwa kosa kubwa, tena ni dhambi inayohitaji toba na msamaha wa Mungu. Hata serikali yoyote duniani inapotunga sheria za kuhalalisha kuua watoto wake, basi ijue inafanya hivyo si tu kwa hasara yake yenyewe, bali hasa kwa imani ya watu wake,” anasema.
Watetezi wa utamaduni wa uhai dhidi ya utamaduini wa kifo wanasema utoaji mimba husababisha kuwakosa watu ambao wangetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi wakiwamo marais, mawaziri, wanasayansi, mabingwa wa tiba, walimu, wakulima na vijana ambao wangelitumikia taifa kama walinzi wa nchi.