DODOMA: SERIKALI imesema utoaji mimba usio salama unachangia vifo vya wajawazito kwa asilimia 10.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel bungeni jijini Dodoma akijibu swali na nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Conjesta Rwamlaza aliyehoji je vifo vitokanavyo na utoaji mimba usio salama vina ukubwa na madhara gani nchini?
Pia alihoji serikali imejipangaje kupunguza vifo vitokanavyo na utoaji mimba usio salama?
“Serikali mlisaini Mkataba wa Maputo ‘Maputo Protocol’ kutetea haki za wanawake na uzazi salama, makubalino hayo yalilenga mimba zitolewe zile za kubakwa, shambulio la ngono, mimba maharimu, serikali haioni umuhimu wa kuweka makubaliano hayo katika sheria za nchi yetu ili kuwasaidia wamama wanaopata mimba za namna hii waweze kuzitoa kwa usalama bila kuhatarisha maisha yao? alihoji Conjesta
Akijibu swali hilo, Dk Mollel amesem tafiti zilizofanywa, matatizo yatokanayo na utoaji mimba ni moja ya sababu inayochangia vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 10.
Amesema madhara yanayotokana na utoaji wa mimba usio salama ni pamoja na uambukizo mkali wa mfumo wa uzazi (Septic Abortion) ambao unaweza kupelekea mgonjwa kutolewa mfuko wa uzazi na wakati mwingine kupoteza maisha.
“Eneo hili ni muhimu lizungumzwe ili kuendela kutoa hamasa kama kuna tatizo na kuna watu wanapoteza maisha sababu ya utoaji mimba usio salama,….; “Duniani kwa mwaka wanawake milioni 42 upoteza maisha na vifo vya utoaji mimba usio salama ni milioni 20 na kidunia ni asilimia 13 wanapata haya matatizo,”amesema Mollel
Aidha amesema, serikali itaendelea kutoa hamasa kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Maendeleo ya Jamii, na wadau wengine ikiwemo kuwataka wabunge wawe mabalozi ili watoto wajue kuna wakati muafaka wa kuanza kushiriki tendo la ndoa.
“Nyie wabunge muwe mabalozi watoto wetu wajue kuna wakati muafaka wa kuanza hayo mambo, wote tukiboresha na kuhamasisha maadili katika jamii yetu ni moja wapo ya sehemu ya kushuka kwa mimba zisizotarajiwa, amesema Mollel
Aidha, akizungumzia Mkataba wa Maputo amesema unahitaji mchakato mkubwa kwa kuwa unagusa wizara mbali mbali lakini unagusa imani mbali mbali za watu na mambo mengine hivyo kuomba wabunge waipe Wizara ya Afya muda ili wachakate mkataba huo.
“Tunaomba mtupe muda tuendelee kuchakata ili tusiwe tunazuia tatizo kwa namna nyingine na kuanzisha tatizo lingine….; “Serikali ipo ‘committed’ na elimu itaendelea kutolewa.
Tanzania ilisaini Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu – Mkataba wa Nyongeza wa Haki za Wanawake Barani Afrika ukijulikana kama Mkataba wa Maputo ‘Maputo Protocal’ ambao ulitungwa kuwa sehemu ya nyongeza ya Mkataba wa Haki za Binadamu na Watu wa Mwaka 1981.
Ujio wa nyongeza ya mkataba huo ulitokana na kuonekana kuna mambo yanakoseka kuhusu haki za Wanawake, ambapo ulisainiwa Julai 2003 na ukaanza kutumika mwaka 2005, lakini kwa Tanzania ulianza kutumika mwaka 2007.
IBARA YA 14 (2c) YA MKATABA WA MAPUTO
Tanzania baada ya mkataba huo mengi yalifanyiwa kazi isipokuwa katika suala hilo la kulinda Wanawake wanaopata ujauzito kwa njia ya ukatili au pasipo kutarajia kama inavyoelezewa katika IBARA YA 14 (2c) ya mkataba huo wa Maputo.
Kipengele hicho kinahusu masuala ya afya ya uzazi hasa katika kutoa mwanya kwa Mwanamke kutolewa/kutoa mimba pale anapokabiliana na mazingira kadhaa ambayo yanaweza kuwa hatarishi kwake.
Kwa Tanzania, Sheria zinaeleza utoaji mimba ni kosa lakini inaruhusiwa kwa masharti ya kuwa ujauzito unahatarisha afya au maisha ya mama.
Lakini katika Mkataba wa Maputo, kuna vipengele vinavyotoa uwanja mpana wa mazingira ya utoaji mimba pale kunapokuwa na uhitaji huo, na baadhi ya nchi ambazo nazo zimesaini mkataba huo na kuutekeleza ni Algeria, Benin, Ethiopia, Liberia, Sierra Leone, Afrika Kusini na Tunisia.