BALOZI wa Uturuki nchini, Dk Mehmet Gulluoglu amesema serikali ya nchi yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala mbalimbali ikiwamo nyanja ya ulinzi na usalama.
Dk Gulluoglu alisema hayo wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya karne moja ya ushindi wa kijeshi taifa hilo lililoupata dhidi ya uvamizi na baadaye kupata uhuru na kulifanya kuwa la demokrasia na usasa.
Aliipongeza Tanzania kwa namna inavyoisimamia na kuilinda mipaka yake dhidi ya magaidi hasa katika mikoa ya Kaskazini na akasema kutokana na uwepo wa urafiki baina ya Uturuki na Tanzania, wamejihakikishia kuendelea kuimarisha ushirikiano huo.
“Tutahakikisha tunaendelea kuimarisha zaidi ushirikiano huu na Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo ushirikiano wa usalama wa kijeshi kwa kuendesha mijadala mbalimbali, programu za mafunzo na misaada ya kijeshi,” alisema Balozi Dk Gulluoglu.
Katika hafla hiyo ilifanyika juzi katika Ubalozi wa Uturuki, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na waambata wa kijeshi wa Jeshi la Uturuki na maofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Dk Gulluoglu alisema anatarajia ushirikiano huo wa ulinzi na usalama utasaidia kuongeza tija katika eneo hilo.
Alisema maadhimisho hayo ni tukio muhimu kwa Uturuki hasa wanapowakumbuka mashujaa wa taifa hilo waliojitolea maisha yao katika uvamizi huo ulioanza mwaka 1919 hadi Agosti 30, 1922 walipopata ushindi.
“Katika tukio hilo zaidi tunamkumbuka Mkuu wa vita hivyo vya uhuru, Ghazi Mustafa Kemal Ataturk, wajumbe wa Bunge la Uturuki pamoja wanajeshi wote ambao walisimama imara na kulipa ushindi mkubwa taifa lao,” aliongeza.
Alisema tangu kuanzishwa kwa Serikali ya Jamhuri ya nchi hiyo mwaka 1923, taifa hilo limeendelea kuwa imara na mjumbe mtiifu katika jumuiya za kimataifa likiwa mshauri na msimamizi wa masuala ya amani na utulivu.
NMB yaipongeza Polisi kudumisha usalama, amani
Na Mwandishi Wetu, Moshi
BENKI ya NMB imesema usimamizi wa Jeshi la Polisi kwenye masuala ya ulinzi na usalama umeiwezesha kuwa kinara wa huduma za kifedha nchini.
Akizungumza mjini Moshi mkoani Kilimanjaro juzi kwenye mkutano wa maofisa waandamizi wa jeshi hilo, Rais Samia Suluhu Hassan alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi kwa karibu na wadau maendeleo zikiwemo taasisi za fedha.
“Tunalipongeza jeshi letu la polisi kwa kuendelea kusimamia usalama na amani nchini ambayo ni msingi mkubwa wa maendeleo wa mataifa yote duniani,” Rais Samia alisema kwenye hotuba yake ya kukifungua kikao kazi hicho kwenye Chuo cha Polisi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, alisema mchango wa NMB kulisaidia Jeshi la Polisi kuwahudumia Watanzania ni wa kuigwa.
Alitoa mfano wa benki hiyo kukubali kugharamia ununuzi wa samani za kituo chake kipya kitakachozinduliwa hivi karibuni Zanzibar.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alieleza mkutano huo benki hiyo itadumisha ushirikiano na Polisi na kulipa kipaumbele ili utendaji kazi wake uendelee kuwa wa ufanisi na tija kwa taifa.
“Ushiriki wa NMB katika ukusanyaji mapato ya serikali ni mkubwa sana. Makusanyo zaidi ya shilingi trilioni 9.6 yalifanyika kati ya mwaka 2018 na 2021 ikiwa mwaka jana pekee tulikusanya shilingi trilioni 3.7. Na kwa Jeshi la Polisi makusanyo kwa mwaka 2021 yalikuwa zaidi ya shilingi bilioni 40,” alisema Zaipuna.
Alieleza washiriki wa mkutano kuwa jeshi hilo lina mchango mkubwa katika mafanikio yao kwa kuiunga mkono kibiashara.
Zaipuna alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kulinda matawi yote 227 ya NMB yaliyo nchi nzima.
Aliliomba Jeshi la Polisi kuendelea kushirikiana na benki hiyo kama mshirika mkubwa wa kifedha na kusaidia serikali kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025.
Pia alisema NMB ina uzoefu na utaalamu wa kukidhi mahitaji ya chombo hicho.
“NMB inaongoza sokoni katika matumizi ya teknolojia kuwahudumia wateja ambapo zaidi ya asilimia 95 ya miamala yake inafanyika kidijitali nje ya matawi kupitia mawakala zaidi ya 10,000, ATMs zaidi ya 800 na huduma nyingine mbadala za kibenki kama NMB Mkononi na Internet Banking,” alifafanua Zaipuna.