MKUU wa Wilaya ya Geita, Colnery Magembe amemsimamisha kazi Mwenyekiti wa Kijiji cha Saragulwa, Kata ya Nyamwillolelwa kwa tuhuma za kusimamia mauziano ya pori tengefu linalomilikiwa na kijiji.
Magembe amechukua hatua hiyokwenye mkutano wa hadhara wa kijiji hicho kufuatia tuhuma zilizotolewa na wananchi na kueleza Mwenyekiti atapisha uchunguzi wa kamati itakayoundwa.
Amesema eneo la pori tengefu walipewa wananchi waliokubali kutoa maeneo yao na kupisha ujenzi wa shule kijijini hapo, lakini baada ya kufika porini kwa ajili ya kulima walikuta baadhi ya watu wanalimiliki.
“Walipoenda kukagua wakakuta Mwenyekiti ameshiriki kwenye mauziano, hakuuza lakini yeye ndiye aliyehusika na kutia muhuri wa kijiji, hili ni kosa kubwa sana la kisheria.
“Mwenye mamlaka kwenye kijiji kugonga muhuri na ikaonekana ni nyaraka halali, ni mtendaji wa kijiji tu, kwenye kitongoji mwenye mhuri ni mwenyekiti wa kitongoji.
“Eneo lile lingekuwa salama, hata wale watu wangekuwa wanataka kulima, wenye maeneo walionyang’angywa kujenga shule, wangekuwa wamepewa kule.
“Kwa sababu Mwenyekiti wanamtuhumu, mimi nitaunda tume ambayo itakuja kuchunguza wapate ukweli, kama mnamsingizia atapata haki yake,” ameelekeza Magembe.
Ameagiza serikali za kijiji kuzingatia utaratibu wa kusoma mapato na matumizi kwa wananchi ili kupunguza taharuki kwenye uendeshaji na usimamizi wa miradi inayojengwa kwa nguvu za wananchi.
“Suala la mapato na matumizi, kila serikali ya kijiji inapaswa kusoma mapato na matumizi ndani ya kipindi cha miezi mitatu na kama haifanyiki hapa, watapata nafasi ya kujibu.
“Mwenyekiti kama huendeshi kijiji kwa uataratibu huo hufai kukaa hapa, kama huwa hauji kusoma mapato na matumizi, hufai kuendelea kuitwa Mwenyekiti,” amesema.