UVCCM Arusha: Gambo aombe radhi

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Arusha umemtaka Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo kutoka hadharani na kuomba radhi kwa kauli waliodai kuwa ni dhihaka na dharau kwa Rais Samia Suluhu na serikali vinginevyo ang’atuke ndani ya chama hicho.

Katibu wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Ibrahimu Kijanga alisema hayo Septemba 19, 2023 jijini Arusha alipozungumza vyombo vya habari na kuongeza kuwa Gambo alisema hayo katika kongamano la elimu mkoa lililofanyika Arusha.

Kijanga alisema Gambo amekosa heshima na nidhamu na kwa muda mrefu amekuwa kirusi ndani ya CCM kutokana na kauli zake tata dhidi ya Rais na viongozi wa serikali walioteliwa na Rais mkoani Arusha kwa kuwa hawana maelewano nao.

Akizungumzia kauli ambayo Gambo ameitoa hivi karibuni katika mkutano wa wakuu wa shule za sekondari, katibu huyo alidai kuwa Gambo amekosa nidhamu kwa kutoa maneno ambayo yamekifedhehesha chama hicho na serikali yake iliyopo madarakani.

“Pamoja na mambo mengine Gambo alizungumza maneno yaliyojaa dhihaka kwa Mh Rais lakini pia kwa wateule wa Rais katika Mkoa wa Arusha ,maneno yale kama Umoja wa Vijana yametufedhehesha ndio maana tukasema tuje kuongea na waandishi wa habari,”

“Kama ataendelea na tabia hiyo tunafikiria kutoa mapendelezo kwa wakuu wa chama ili yaweze kufanyiwa kazi maana sio mara moja akiwa anawabeza viongozi wa chama na serikali mkoani Arusha.’’ Alisema Kijanga.

Maneno yanayodaiwa kusemwa na Gambo ni kwamba kazi ya mbunge ni kuwatumikia wananchi ila kazi ya wateule wa Rais ni kumfurahisha aliyewateua kwa kuimba nyimbo za mapambio.

“Naamini Gambo alikuwa DC na baadaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa ina maana alikuja kuimba mapambio sisi tunaamini kwamba wateule wote walioletwa na Mh Rais wanakuja kuwatumikia watanzania”

Katibu Kijanga aliendelea kusema kuwa wateule wote wa Mkoa wa Arusha walioletwa na Rais na Mwenyekiti wa CCM  aliyechaguliwa na wana CCM wamekuja Arusha kuwatumikia Watanzania na kama kuna changamoto Rais huwa anaziona na kuzifanyia kazi na sio kama anavyofikiria yeye.

Alisema UVCCM inamkemea Gambo kuacha mara moja kauli za dhihaka na dharau kwa Rais na wateule wake na ajifunze lugha za staha na ajifunze tamaduni za kuongea na kama hataki kuwepo ndani ya Chama Cha Mapinduzi anapaswa kung’atuka tu

Katibu wa UVCCM Mkoa wa Arusha alisema kuwa Jumuiya hiyo inamtaka Gambo kuacha mara moja kauli za kejeli, kauli za dhihaka kauli za dharau aziache na kusema watanzania hawana uhuru na wananyimwa kuongea ukweli na serikali inatumia mabavu kuongoza watanzania kauli hizo anapaswa kuziacha kwani serikali ya Rai Samia inafanya kazi nzuri .

Alisema UVCCM Mkoa wa Arusha inatoa ushauri kwa uongozi wa CCM Mkoa wakati umefika kuchukua hatua dhidi ya mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwani anaona kama anabanwa ndani ya chama ili aweze kwenda kuwatumikia wananchi sehemu nyingine na sio kwa mwavuli wa CCM.

Habari Zifananazo

Back to top button