UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Wilaya ya Nyamagana, umewataka wakazi wa wilaya hiyo, washiriki kikamilifu kwenye sensa ya watu na makazi pamoja na kutoa taarifa sahihi.
Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa UVCC Wilaya ya Nyamagana, Boniphace Zephania, wakati wa Tamasha la kuhamasisha Sensa lililofanyika viwanja vya Ndama mkoani hapa.
“Sisi hapa Nyamagana tayari vifaa vya sensa vimeshafika, hivyo nitoe rai kwa Watanzania tujitokeze kwa wingi, ili zoezi letu liweze kufanikiwa,” amesema Zephania.
Amesema UVCCM Nyamagana, wameandaa oparesheni malumu siku ya sense, ili kuhakikisha wananchi wote wanajitokeza kuhesabiwa.
Kwa upande wake Katibu wa CCM wilaya ya Nyamagana, Godfrey Kavenga, amesema wanaunga mkono sensa, kwani ipo katika Ilani ya Uchaguzi, huku akitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa sahihi kwa makarani wa sense.