UVCCM wafunda vijana kilimo biashara
UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Ulanga , mkoani Morogoro umewataka vijana nchini wakiwemo wasomi kujitokeza kutumia fursa za uwezeshwaji kiuchumi zinazotolewa na serikali kuanzisha miradi ya kujiajiri ikiwemo kwenye kilimo biashara ili waondokane na kulalamika kuhusu ukosefu wa ajira.
Katibu wa Hamasa na Chipukizi UVCCM Wilaya ya Ulanga, Thomas Machupa alisema hayo mjini Morogoro akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya tamasha la kumpongeza Rais, Dk Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Ulanga, Salim Alaudin Hasham kwa namna alivyowezesha vijana kiuchumi na kujiajiri ambalo litafanyika Juni 10,2023
Machupa alisema imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa makundi mbalimbali likiwemo la vijana ili kunufaika na fursa zinazotolewa ikiwemo ya mikopo ya asilimia 10 kupitia halmashauri za wilaya .
Alisema katika asilimia hizo kundi la vijana limetengewa asilimia nne, kundi la wanawake nalo limetengewa asilimia nne, wakati wenye ulemavu wao wametengewa asilimia mbili.
Alisema kutokana na mikopo ya asilimia nne iliyokuwa ikitolewa kwa kundi la wanawake, vijana na asilimia mbili kwa wenye ulemavu, vikundi zaidi ya saba vya vijana vimefanikiwa kupata mikopo hiyo kwenye sekta ya kilimo cha vitunguu na matikiti ikiwa na kupatiwa Pikipiki (bodaboda) 65, ambapo kiwango kikubwa cha mikopo hiyo imerejeshwa.
Machupa alisema, malengo ya vijana wa wilaya hiyo ni kuinuka kiuchumi , hivyo viongozi wa serikali ya wilaya na halmashaurui wanao wajibu wa kuwapatia maeneo zaidi kwa ajili ya kilimo mkakati cha mazao ya chakula na biashara.
Hivyo alisema serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha ina tekeleza Ilani ya CCM , imeweza kuwafikia vijana wengi kwa kuwagusa moja kwa moja kwenye suala la kuwapatia mikopo isiyo na riba kwa vikundi vyao kupitia halmashauri .
“Huu ni wasaa sasa wa vijana wakiwemo wa CCM kuacha kulalamika kwani kila sehemu tunaonekana ni watu wa kulalamika, lakini tunatakiwa kushukuru kwa hata tunachokipata ili upate vingi inabidi ushukuru kwanza kwa ulichokipata,”alisema Machupa
Machupa alisema katika tamasha la kumpongeza Rais, Mbunge na Serikali kwa ujumla limelenga kutambua namna moja ama nyingine kuhusu maendeleo yaliyofanyika kwa Mkoa wa Morogoro hususani Wilaya ya Ulanga ,kitendo kilichowafanya vijana sasa kujitambua na kujituma kufanya kazi kwa bidii.
Naye Katibu wa UVCCM wa wilaya hiyo, Rukia Makoja alisema umoja huo una kila sababu ya kujivunia miradi ya maendeleo inayofanyika nchini ikiwemo ya ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, pamoja na shule za msingi na sekondari.
Kwa upande wake Mwenyekti wa UVCCM wa wilaya hiyo, Shaista Kuyela ,alisema mgeni rasmi kwenye tamasha hilo anatarajiwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Rehema Sombi.
Kuyela ,alisema tamasha hilo linatarajia kufanyika Juni 10, mwaka huu (2023) na litashirikisha vijana zaidi ya 2,500 kutoka tarafa nne za wilaya hiyo ambazo ni Lupilo, Ruaha, Mwaya na Vigoi ambalo litambatana na maandamano ya amani na shughuli za kufanya usafi maeneo ya umma na kutoa msaada kwa watoto yatima wa kituo cha Ukwama.