Uwanja mpya Arusha kutumika PAMOJA AFCON 2027

BUNGENI, Dodoma: SERIKALI kujenga Uwanja wa kisasa wa michezo jijini Arusha ikiwa ni ukamilisho wa viwanja vitatu nchini vitakavyotumika katika Fainali za Mataifa Afrika (PAMOJA AFCON 2027).
Akizungumza leo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amewatoa hofu Watanzania juu ya maandalizi kuelekea PAMOJA AFCON 2027 ikiwa ni ushirikiano wa mataifa ya Kenya, Uganda na Tanzania.
“Lakini kabla ya PAMOJA AFCON, Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu Septemba nchi hizi tatu zitakuwa wenyeji wa pamoja wa michuano ya CHAN (michuano ya Mataifa Afrika kwa wachezaji wanaohudumu ndani ya bara la Afrika),” amesema Dk Ndumbaro.
Amesema wanatumia michuano ya CHAN kuwa sehemu ya maandalizi kuelekea PAMOJA AFCON ambapo Tanzania itakuwa na vituo viwili, Zanzibar katika Uwanja wa New Amaan complex na Dar es Salaam katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, ulio katika ukarabati unaotarajiwa kukamilika Agosti, 2024.
Amesema kuelekea PAMOJA AFCON, Tanzania itatumia viwanja vitatu ambavyo ni Uwanja wa Benjamin Mkapa wa jijini Dar es Salaam, New Amaan complex wa visiwani Zanzibar na Uwanja mpya utakaojengwa jijini Arusha.
“Tunategemea ndani ya mwezi huu wapili mkandarasi atakabidhiwa ‘site’.” Amesema kiongozi huyo.
Dk Ndumbaro amesema kutokana na uwenyeji wa nchi tatu, wamekubaliana jina litakalotumika ni PAMOJA AFCON.

Habari Zifananazo

Back to top button