ZAIDI ya mifugo 36000 iliyopo jijini Tanga, inatarajiwa kutambuliwa kwa kuwekewa alama ya hereni za kielektroniki.
Akizungumza baada ya kuzindua uwekaji herein huo, Mkuu wa wilaya ya Tanga, Hashim Mgandilwa, amesema kuwa hatua hiyo itasaidia serikali kujua idadi ya wanyama waliopo nchini, hivyo kurahisisha ugawaji wa dawa na pembejeo za mifugo.
“Kutokana na sisi tupo katika maeneo ya mipakani, kuna muingiliano wa wanyama, hivyo kwa zoezi hili tutambua mifugo yetu na hivyo itaweza kuwa salama tofauti na sasa,”amesema Mgandilwa.
Naye Ofisa Mifugo na Uvuvi wa Halimashauri ya Jiji la Tanga, Dk Paul Kisaka, amesema katika zoezi hilo wamejipanga kuweka hereni mifugo zaidi ya 36,000 .
“Tunatarajia kuweka hereni kwa ng’ombe takribani 32,000,mbuzi 4,500 pamoja na punda 320, hayo ndio matarajio yetu, hivyo niwaombe wafugaji wajitokeze kwa wingi kuleta mifugo yao iweze kuwekewa herein,”amesema Kisaka.