MAMLAKA ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imesema uwekezaji kampuni za Said Salim Bakhresa Dola za Marekani milioni 253.3 (sawa na Sh bilioni 595) visiwani Zanzibar umewezesha kupatikana ajira 1,228.
Mkurugenzi Mtendaji wa Zipa, Sharrif Ally Sharrif ameipongeza kampuni hiyo kwa kuichagua Zanzibar kuwa kituo cha uwekezaji wao katika miradi tofauti. Sharrif amesema hayo Unguja kabla Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi hajaizindua boti ya Kilimanjaro VIII na akaitaja miradi hiyo ni pamoja ya usafiri wa baharini, hoteli, makazi eneo la Fumba, viwanda na nishati.
Alisema katika kipindi cha miaka miwili na nusu ya uongozi wa Dk Mwinyi hadi mwezi uliopita, Zipa imesajili miradi 232 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 3.54 zikiwamo hoteli, viwanda, kilimo, nishati, maendeleo ya majengo nk.
Sharrif alisema miradi hiyo inatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja zaidi ya 13,500 na akasema kuongezeka kwa uwekezaji visiwani humo kutawezesha kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla. Awali kampuni ya Azam Marine iliishukuru na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji yaliyoiwezesha kuwekeza dola za Marekani mil 120 katika usafiri wa baharini.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Aboubakar Salim Bakhresa alisema kampuni hiyo imetoa ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya wafanyakazi 400 na inasafirisha takribani watu 2,000,000 kwa mwaka kati ya Tanzania Bara na Zanzibar wakiwamo raia wa kigeni 180,000.
Alisema idadi hiyo ni sawa na abiria 5,000 wanaohudumiwa kwa siku moja na akasema vyombo vyao vina uwezo wa kusafirisha abiria 11,500 kwa siku moja hasa wakati wa sikukuu. Salim alisema tangu mwaka 2010, Azam Marine wamelipa kodi na tozo Sh bilioni 130.
Alisema boti ya Kilimanjaro VIII imejengwa kwa miezi 18 nchini Australia ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 631 kwa wakati mmoja.
Salim alisema boti hiyo ina madaraja matatu likiwamo la kawaida abiria 559, VIP abiria 56, Royal class abiria 16 na nauli zinabaki kama za sasa.