UWEKEZAJI wa ubanguaji wa korosho nchini unaendelea kufanyika ili kuhakikisha uwepo wa ajira kwa vijana na wanawake.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dk Geofrey Mkamilo amesema hayo katika maonesho ya Kitaifa ya sikukuu ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yaliyohitimishwa jana mkoani Mbeya na Rais Samia Suluhu Hassan.
Dk Mkamilo amesema uwekezaji huo wa ndani ni mikakati ya kuhakikisha korosho zinabanguliwa ndani isiwe tu kwa asilimia 10 iliyopo, bali asilimia iongezeke kutoa ajira nyingi zaidi hapa nchini kuondoa changamoto ya kutokuwa na ajira.
“Sasa hasara ya kubangua kwa kiasi hicho kidogo maana yake ni kwamba ajira unaipeleka nje, lakini la pili ni kwamba unapobangua nje maana yake wale watu wataongeza thamani kwenye zao letu tunalouza nje na hii inasababisha kwamba wenzetu wanapata faida zaidi kwa sababu wao wanabangua kule nje,” amesema.
Amesema kaulimbiu ya nanenane mwaka huu, “ Vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula.’ Kwa kauli mbiu hiyo inabidi uwekezaji wa kubangua korosho uongezeke kwa wingi nchini.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Naliendele kilichopo Mtwara, Dk Fortunus Kapinga amesema nchi iende kwenye dhana ya kutaka kubangua korosho zake ili kuongeza thamani ndani ya nchi.
“Unaweza kuongeza thamani kwa kubangua korosho, kuongeza thamani baada ya kubangua kwa kutengeneza bidhaa nyingine.
“Imefika mahali TARI tunaongezea thamani korosho zilizoongezewa thamani kwa mfano korosho ulizobangua inawezekana imevunjika ikawa vipande vipande ambapo bei inakuwa sio nzuri, hapo unaweza kupata bidhaa nyingine ikawa mara tatu ya bei iliyopo,” amesema.
Amesema kupitia korosho zilizovunjika inawezekana kutengenezea siagi, maziwa ya korosho na bidhaa nyingine.
Kwa upande wake Mratibu wa zao la korosho kitaifa kutoka TARI Naliendele, Dk Wilson Nene amesema hivi sasa zinaongelewa tani 189,000 za uzalishaji wa korosho ghafi.
“Kwa takwimu tulizonazo tuko kati ya asilimia 10 mpaka 20 ya korosho ambayo tunaiongezea thamani hapa nchini Tanzania lakini lengo ni kuwa ifikapo 25/26 tufikishe asilimia 60 ya uongezaji wa thamani wa korosho yetu kutokana na uzalishji wa mwaka huo,” amesema.
Amesema mwaka 2025 inategemewa uzalishaji wa korosho kufikia tani 700,000, ina maana katika tani hizo asilimia 60 ihakikishe zimebanguliwa.
Comments are closed.