Uwepo mjadala kitaifa kabla ya Katiba mpya

Uwepo mjadala kitaifa kabla ya Katiba mpya

KIKOSI Kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kimependekeza kuwepo na mjadala wa kitaifa ili kupata mwafaka katika masuala ya msingi kabla ya kuanza mchakato wa kuanza kuandika Katiba mpya.

Akiwasilisha ripoti kwa Rais Samia jana, Mwenyekiti wa Kikosi Kazi hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema mjadala huo ufanyike kwa ushiriki mpana wa wananchi.

Masuala ya msingi yanajumuisha muundo wa muungano, madaraka ya rais, mfumo wa uchaguzi, madaraka ya serikali za mitaa, masuala ya rushwa, maadili na mengine yatakayojitokeza.

Advertisement

Alisema jambo jingine la kuzingatia ni kuhuisha sheria ya mabadiliko ya katiba na sheria ya kura ya maoni ili kuweka mahitaji ya sasa ikiwemo kuainisha muda wa mchakato mzima, kutambua kuanzishwa kwa jopo la wataalamu na kuainisha misingi ya kuzingatiwa katika mchakato wa mabadiliko ya katiba.

Kikosi kazi hicho pia kimependekeza kuwapo kwa ushirikishwaji mpana wa wananchi katika mchakato wa kuhuisha sheria hiyo kwa kufuata taratibu za utungaji wa sheria nchini.

“Tunapendekeza kwamba baada ya sheria ya mabadiliko ya katiba kuhuishwa, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar, aunde jopo la wataalamu litakalopitia na kuoanisha katiba inayopendekezwa na rasimu ya pili ya katiba iliyoandaliwa na tume ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011 na kuandaa rasimu ya katiba mpya itakayowasilishwa bungeni,” alisema Profesa Mukandala.

Kikosi Kazi kinapendekeza kuwa katika utekelezaji wa majukumu yake, jopo la wataalamu lifanye mapitio ya katiba inayopendekezwa ya mwaka 2014 kwa kuzingatia hali ya sasa kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Mapendekezo ni kwamba rasimu ya katiba mpya ipitishwe na bunge baada ya jopo la wataalamu kumaliza kazi yake. Elimu ya uraia kuhusu katiba inayopendekezwa itolewe kabla ya kupigiwa kura ili wananchi waifahamu katiba husika na hatimaye wapigie kura ya maoni katiba inayopendekezwa.

Kwa mujibu wa Profesa Mukandala, Watanzania walionekana kugawanyika katika makundi mawili kuhusu suala la katiba mpya kwa kuwa wapo wanaoamini kuwa hakuna haja ya katiba mpya badala yake iliyopo ifanyiwe marekebisho. Wengine waliamini kuwa kuna haja ya kuwa na katiba mpya.

Profesa Mukandala alisema Watanzania walionekana kugawanyika katika makundi matano kuhusu njia mwafaka ya kupata katiba mpya.