Uwindaji wa kienyeji wasubiri kanuni

Uwindaji wa kienyeji wasubiri kanuni

WIZARA ya Maliasili na Utalii imewatoa wasiwasi Watanzania kuwa vibali kwa ajili ya uwindaji wa kienyeji vitatolewa baada ya mchakato wa kupitia kanuni za uwindaji wa wenyeji na wageni kukamilika.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Sikonge, Geroge Kakunda (CCM).

Kakunda alitaka kufahamu ni lini vibali vitatolewa kwa ajili ya uwindaji wa kienyeji kwa ajili ya manufaa ya wananchi.

Advertisement

Akijibu swali hilo, Masanja alisema mchakato wa kupitia kanuni za uwindaji huo umeshafika kwa waziri na karibuni yatatoka maelekezo ya utekelezaji wake.

Kwa mujibu wa Masanja, serikali iliona changamoto ya kuwakosesha haki wananchi ya kupata vitoweo vya wanyamapori na ndio maana walikuwa na mchakato wa kupitia kanuni hizo na kuwa zikipitishwa huenda hata gharama ikapungua.

Katika swali la msingi Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka (CCM) alitaka kufahamu lini vibali vya uwindaji vitatolewa.

Akijibu swali hilo, Masanja alisema uwindaji wa wanyamapori umegawanyika katika makundi mawili ambayo ni uwindaji wa kitalii na uwindaji wa wenyeji au wageni wakazi.

Masanja alisema uwindaji wa kitalii ambao unalenga kupata nyara kwa ajili ya watalii unasimamiwa kwa kuzingatia Kanuni za Uwindaji wa Kitalii na pia uwindaji wa wenyeji na wageni wakazi hufanyika kwa ajili ya kitoweo na unasimamiwa kwa kuzingatia kanuni za uwindaji wa wenyeji na wageni wakazi.

Kwa mujibu wa Masanja vibali vya uwindaji wa kitalii vinaendelea kutolewa kwa mujibu wa Kanuni husika ambapo hadi sasa jumla ya minada saba imefanyika na wadau wamepewa vibali vyao.

Kwa upande wa uwindaji wa wenyeji na wageni wakazi, vibali hivyo vitaanza kutolewa mara baada ya mapitio ya kanuni za uwindaji wa wenyeji na wageni wakazi kukamilika.