MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Njombe. Scolastika Kevela, amempongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuondoa zuio la kufanyika kwa mikutano ya vyama vya siasa nchini ambayo kwa kipindi kirefu ilikuwa imezuliwa.
Akizungumza Dar es Salaam leo, Scolastika amesema hatua hiyo ya Dk Samia inaonesha busara na hekima alizonazo katika uongozi na kusisitiza kuwa katika kipindi cha karibu miaka miwili tangu aanze kuingoza Tanzania, amefuta machozi ya wanasiasa wengi waliokuwa wakilia kuzuiwa kwa mikutano hiyo.
“Huyu ndiyo Mama, kwa hakika Rais Dk Samia uongozi wake umeonesha alama kubwa hapa nchini, kitendo hiki alichokifanya siyo kitampa heshima hapa Tanzania bali duniani kote kwa kuwa siasa ni kitu kinachotambulika kila mahali,” amesema Scolastika
Akizungumza na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa katika Ikulu Dar es Salaam jana, Rais Samia alitangaza kuondolewa kwa zuio la kufanyika kwa mikutano hiyo ya vyama vyote vya siasa kwa kusema hiyo ni haki yao kikatiba huku akivitaka kuheshimu taratibu za sheria juu ya taratibu za uendeshaji wa mikutano yao.
“Wajibu wenu ni kufuata sheria zinavyosema ni kufuata kanuni zinavyosema, lakini kama waungwana kama wastaarabu Watanzania wenye sifa ndani ya Dunia hii niwaombe sana, tunatoa ruhusa twendeni tukafanye siasa za kistaarabu, siasa za kupevuka, tukafanye siasa za kujenga sio kubomoa.” amesema Dk Samia.
Pamoja na hilo Dk Samia Rais Dk Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inadhamiria kukwamua mchakato wa marekebisho ya Katiba kwa namna watakavyokubaliana na vyama vingine vya upinzania.
“Kuna haja ya kuangalia hali halisi ya sasa hivi, je yale yaliyomo mule mangapi yanatufaa na mangapi hayatufai, tunakwendaje, lengo ni kuona tunafika mahali pale tulipokusudia ” amesema Rais Dk Samia.
Amesema muda wowote kuanzia sasa itaundwa kamati maalumu ambayo itashauri namna ya kuendesha mchakato huo ambayo itahusisha watu wa makundi mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa, vya kijamii, Watanzania walioko International Communities, Wawakilishi wa vyombo vya usalama, watakuwemo kwenye hiyo kati ili waje na kitu ambacho kitakuwa cha Watanzania.”ameongeza Rais Dk Samia.