UWT yataka viongozi wa kuipa ushindi 2024, 2025

UMOJA wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) umeagiza wanachama wanaochaguliwa kuongoza umoja huo katika mikoa wajitoe, wawajibike kuutumikia na kuitetea CCM ishinde Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.
Akizungumza katika Mkutano wa Uchaguzi UWT Mkoa wa Dodoma, Katibu wa UWT Taifa, Dk Philisy Nyimbo alisema kila atakayechaguliwa anatakiwa kuunga mkono juhudi za serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kusaidia Watanzania.
Nyimbo aliagiza watakaoshinda wawaunganishe wanawake katika ngazi mbalimbali kuanzia kwenye mashina, matawi, kata, wilaya, mkoa hadi taifa.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Christina Mndeme alisema viongozi watakaochaguliwa watambue wanakwenda kuunda jeshi kubwa kuanzia ngazi ya matawi, kata, wilaya na mikoa.
Mndeme alisema wanawake hao wanapaswa kuunga mkono juhudi za Rais Samia kuboresha huduma katika sekta za afya, maji, umeme, barabara, demokrasia na hadi ushirikiano wa kimataifa.
Aliagiza washindi mikoani wakiimarishe chama kwenye matawi na ngazi za juu, pia wakahudhurie vikao na wakaongeze idadi ya wanachama kutoka 94,000 wa sasa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema Rais Samia amefanya mengi katika Mkoa wa Dodoma yakiwamo ya kutoa fedha kutekeleza miradi yenye lengo la kuwasaidia wanawake.
Mwenyekiti anayemaliza muda wake na anagombea tena, Neema Kajure aliwapongeza wanachama kwa ushirikiano uliofanikisha kuibua na kutekeleza miradi mingi katika kipindi chao cha uongozi miaka mitano.
Wagombea wengine ni Kaundime Masasi, Elizabeth Lameck na Zabibu Mafiti.
Wakati huohuo, wagombea watatu, Flora Zelothe na Neema Mollel na Muna Taribu wamechuana kuwania uenyekiti wa UWT Mkoa wa Arusha.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Arusha anayemaliza muda wake, Yasmine Bachu alishukuru kwa ushirikiano waliompa katika kipindi cha miaka mitano.
Bachu aliomba viongozi wataochaguliwa walinde uchumi kwani siasa bila uchumi haiwezekani kuendelea.