Uzalendo wawezesha ukuaji makusanyo TRA

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa mafanikio ya ukusanyaji mapato unatokana na uadilifu na uzalendo unaooneshwa na wananchi kwa nchi yao.

Hayo yalisemwa na Kamishna wa TRA, Alfayo Kidata kwenye mahafali 54 ya kidato cha sita ya Shule ya Vipaji ya Kibaha ambapo aliwakilishwa na Stephan Kauzeni. Kidata alisema kuwa nchi yoyote ili iweze kufanikiwa kwenye ukusanyaji mapato lazima walipakodi wawe na uzalendo na kuonyesha uadilifu ambapo ukusanyaji utaongezeka.

“Mapato ndani ya nchi yana kazi nyingi kwenye shughuli za maendeleo hivyo wananchi wanapaswa kulipa kodi kwa uaminifu ili miradi ya kijamii iweze kutekelezwa,” alisema.

Advertisement

Kidata alisema makusanyo yanapokuwa makubwa miradi ya maendeleo nayo inakuwa mingi ikiwa ni pamoja na elimu, afya, miundombinu, maji na huduma muhimu za kibinadamu.

“Tunawaomba wananchi na wafanyabiashara walipe kodi na watu wakinunua bidhaa wahakikishe wanapewa risiti na matumizi ya mashine za EFD ili kuboresha ukusanyaji mapato,” alisema Kidata.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, George Kazi alisema kuwa shule hiyo imeendelea kufanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha sita ambapo walipata daraja la kwanza na la pili.

Kazi alisema kuwa mbali ya mafanikio changamoto kubwa ni upungufu wa maji ambapo wanahitaji matangi 40 ya lita 10,000 kwa ajili ya kuhifadhia maji ambapo kwa siku wanahitaji maji lita 300,000 na yanayopatikana ni chini ya lita 100,000 na maji yanapatikana kwa mgao. Naye Meneja wa Idara ya Elimu ya Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Dk Rodetius Shemlekwa alisema kuwa anaishukuru TRA kwa kukusanya mapato makubwa ambapo yamesaidia elimu ya msingi bila ya malipo.