Uzalishaji umeme bwawa la Nyerere wakaribia
MRADI wa Kufua Umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) umekamilika kwa asilimia 78.68 huku hatua ya kufunga lango la njia ya mchepusho wa maji ikiwa imefi kiwa kwa lengo la kuruhusu ujazaji maji katika bwawa tayari kwa umeme kuanza kuzalishwa.
Hatua hiyo itafuatiwa na kuwasha mitambo baada ya kujaa kwa bwawa, hatua inayotarajiwa kuchukua misimu miwili ya mvua. Bwawa hilo linatarajiwa kukamilika na kuanza uzalishaji Juni mwaka 2024.
Litagharimu Sh trilioni 6.5 hadi kukamilika kwake. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa keshokutwa kuzindua hatua ya kuanza kujaza maji katika bwawa hilo lenye ukubwa wa meta za ujazo 32.3, hafla itakayofanyika katika eneo la mradi huo, Rufiji mkoani Pwani.
Akizungumzia uzinduzi, Waziri wa Nishati, Januari Makamba aliwaambia waandishi wa habari kuwa katika kutekeleza mradi huo, kumekuwa na vipindi vyenye hatua mbalimbali zilizokuwa zikitekelezwa na ujazaji maji ndiyo hatua muhimu kuliko kuliko zote.
“Kama mnavyofahamu kuwa mradi huu una maisha na katika maisha yake kuna alama, vituo mbalimbali ambavyo vinafikiwa kwa vipindi ambavyo ni muhimu, sasa hivi tumefikia kwenye mafanikio makubwa kuliko yote tangu tuanze ujenzi na yenyewe ni kujaza maji kwenye bwawa,” alisema.
Makamba alisema Rais Samia atabonyeza kitufe kitakachoshusha mageti yatakayoziba mchepusho wa maji na kuruhusu maji kuingia katika bwawa hilo.
“Tunayo furaha na fahari kuwatangazia kuwa tumefika hatua hiyo na kutokana na ukubwa na umuhimu wa hatua hiyo na ishara ya mradi kwa maendeleo ya nchi, hatua hii itazinduliwa na Rais (Samia) Desemba 22 mwaka huu,” alisema.
Alisema awali wakati wa kujenga tuta kwa ajili ya kuruhusu uhifadhi wa maji kwenye bwawa hilo, ilikuwa ni lazima kuchepusha maji kuelekea upande mwingine ili kubaki na sehemu kavu, kazi ambayo ilifanyika miaka mitatu iliyopita kwa gharama ya Sh bilioni 235.
Alisema katika hatua hiyo lilitengenezwa handaki lenye urefu wa meta 700 lililowezesha kujengwa kwa tuta kwa ajili ya kusaidia uhifadhi wa maji kwenye bwawa ambalo limekamilika na mageti kwa ajili ya kuziba mchepusho wa maji yameshafungwa katika eneo husika na kuruhusu maji kujazwa. “Kwa tukio hilo maji yataanza rasmi kujaa kwenye bwawa hilo,” alisema.
Tukio hilo litahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa na wananchi wanaotarajiwa kufikia 2,000. Pia kutakuwa na ujumbe wa watu 300 kutoka Serikali ya Misri wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi hiyo ambayo ndiyo wanatoka wakandarasi wa mradi huo.
Makamba alisema hatua hiyo haitazuia maji ya mto Rufiji kwenda upande wa pili kwa ajili ya matumizi mengine ya ikolojia na kwa watu wengine kutokana na muundo wa mradi ulivyo.
Alisema mradi huo una faida nyingi ikiwa ni pamoja kilimo kwa sababu utazuia mafuriko yaliyokuwa yakisababisha mazao kuharibika awali na kuanzia sasa maji yatakayoelekea upande wa chini kwa wakulima yatakuwa yamedhibitiwa na kufika kwa kiwango kinachostahili.
Mradi huo unatarajiwa kuzalisha megawati 2,115 zitakazoongeza nguvu katika megawati 1,500 zinazozalishwa na vyanzo mbalimbali vya sasa na kuondoa tatizo la uhaba wa umeme nchini.
Ongezeko hilo la megawati 2,115 litawezesha Tanzania kujitosheleza kwa mahitaji yake ya umeme na kuwa na ziada ya kuuzwa nchi jirani sambamba na kupunguza gharama za umeme kwa Watanzania.