Uzazi wa mpango unakupa raha, utaepuka karaha

Unaokoa uhai, kupunguza msongo wa mawazo

 “UZAO wangu wa kwanza nilihangaika sana maana mume alipoona amenipa mimba, akakimbia. nilihangaika peke yangu na mimba hadi nikajifungua. mwanaume alipoona nimejifungua salama na ninaendelea na maisha, akarudi,” anasema Esther Emmanuel (20, si jina halisi) mkazi wa Machinjioni, Sengerema Mkoa wa Mwanza.

Esther anayefanya biashara ya kuuza karanga kwa kutembeza mitaani anasema: “Kwa sasa naishi na mume wangu Kikombe Sahani (si jina halisi) na watoto wawili; mkubwa ana miaka sita na mwingine ana miaka miwili.”

Mwanamke huyo katika mazungumzo na HabariLEO kuhusu  uzazi wa mpango na huduma baada ya mimba kuharibika, anasema baada ya kuona hali ilivyo katika uzao wa kwanza, jirani yake alimshauri atumie uzazi wa mpango.

“Nilimwambia siwezi maana mume wangu alishakataa… Kuna kipindi mtoto wangu aliugua sana, lakini mwanaume akakimbia tena, yaani ni misukosuko tu, mtoto alipopona akarudi, ” anasema.

Swali: Kwa nini alikuwa anakimbia?

JIbu: “Mume wangu hana kipato, ni mkulima wa vibarua vya watu, anakimbia majukumu  yake ikifika suala la watoto anakwambia hana hela, kuna wakati ananifukuza anasema haniitaji, mimi navumilia tu sababu ya Watoto ili wakue, maana hata nikisema naondoka naenda wapi? Mama yangu alinifukuza nyumbani nilipopata mimba yam toto wangu wa kwanza.”Anasema

Swali: Je Mmefunga ndoa?

Jibu: Hapana hatujafunga ndoa, tunaishi tu nyumbani kwao, nilipobeba mimba nilifukuzwa na mama alisema hawezi kunilea mimi na mtoto wangu, nikaenda kwao mwanaume, nashukuru walinipokea ndio tunaishi hivyo hivyo tu kishida shida.

“Tulikaa kama miaka mitatu hivi, nikabeba tena mimba. Hii sasa ilikuwa mimba ya pili kama kawaida, mwanaume hanijali wala hajali mtoto wala hanijali.”

“Ndipo jirani akanishauri tena, nitumie njia ya uzazi wa mpango ili nisibebe tena mimba bila kutarajia Ikabidi nikubali. Nikaamua kutumia uzazi wa mpango; nikachomwa sindano, nilianza mwezi wa pili mwaka huu, nataka nileee wanangu wakue.”

Katika mazungumzo hayo na Esther anabainisha kuwa, awali alikuwa analelewa na bibi na babu na kuwa aliacha shule akiwa darasa la pili kutokana na kusumbuliwa na macho.

“Nilipofikisha miaka 13, mama alinichukua nikaenda kuishi naye Geita, baada ya mwaka mmoja, nikabeba mimba mama akanifukuza eti hawezi kuishi na mimi akanipeleka kwa mwanaume aliyekuwa amenipa mimba,” anasema.

 Anasema kwa kuogopa mkono wa sheria kwa kosa la kumpa ujauzito mwanafunzi, mwanaume huyo (Kikombe) akakimbia na kuwa anaonekana mara moja moja.

“Mara aonekane, mara asionekana,” anasema Esther na kuongeza:

 “Akawa anaishi kama digidigi; akawa anakuja mara moja moja usiku kwa usiku, nikajikuta nabeba tena mimba ya pili; na yenyewe akaikataa kwa madai kuwa si mimba yake.”

Anasema alilazimika kuvumilia hali hiyo hadi alipojifungua na Kikombe kupata taarifa za Esther kujifungua akarudi nyumbani na kumtaka aondoke kwa kuwa hawezi kulea mtoto asiye wake.

“Nilivumilia maneno hayo ya kila siku, lakini kuna siku alichachamaa kunifukuza eti mtoto si wake; kwa kweli nikagoma kuondoka; nikasema siondoki nitabaki hapahapa wanangu wakue, wakikua nitajua cha kufanya,” anasema.

Anasema kilichokuwa kinamshangaza ni kuwa, Kikombe Sahani hakuwa anataka Esther atumie njia yoyote ya uzazi wa mpango, lakini kila anapopata ujauzito inakuwa nongwa, anamkimbia au kumtaka aondoke nyumbani eti mimba si yake.

“Aligoma nisitumie njia yoyote ya uzazi wa mpango, hivyo nikaamua kuchoma sindano kimya kimya,” anasema Estha na kuongeza: “Ndio maana nawashauri vijana wenzangu kutumia njia za uzazi wa mpango ili kuepuka mimba zisizotarajiwa, ili watimize malengo yao,” anasema.

Happiness John naye anazungumzia kuhusu uzazi wa mpango na kueleza kuwa jamii imekuwa na  mtazamo hasi kuhusu uzazi wa mpango.

“Watu wengine katika jamii wanaamini kuwa njia hizo husababisha ugumba kwa wanawake, ukweli ni kwamba, njia za uzazi wa mpango hazisababishi ugumba, labda tu mtu akizitumia bila  kufuata utaratibu na ushauri na maelekezo ya wataalamu,” anasema.

Anatoa ushuhuda wake akisisitiza kuwa, njia za uzazi wa mpango hazina tatizo na yeye amezitumia kwa takribani mwaka sasa na yuko vizuri.

“Nilipoanza kutumia niliambiwa nisifanye kazi nzito sijapata shida yoyote, siku zangu naingia kama kawaida, na sijapata shida yoyote sasa ni mwaka na kitu,” anasema Happiness.

Anasema kilichomsukuma kuanza kutumia uzazi wa mpango na kubaini faida ya uzazi huo ni ujauzito alioupata na kuharibika.

“Mwanzoni nilipata kipindi kigumu sana; nikajiuiliza itakuwaje hospitali wakisema nimetoa mimba na manesi nitakaokutana nao watanipokea vipi?”Anahoji.

Anafafanua kuwa  alikuwa na mimba ya miezi mitatu. “Siku moja nikahisi tumbo linauma. Sikulitilia maanani lakini, baada ya siku tatu maumivu yakazidi; nikaanza kuona damu.”

“Nikaamua tu, kwenda Kituo cha Afya Katunguru iliyopo wilaya ya Sengerema nilipata huduma nzuri nikafarijika ingawa mwanzo nilihofia kukaripiwa nimetoa mimba. Wakaniambia mimba imetoka.

“Wakanisafisha na kunishauri kuanza uzazi wa mpango. Huduma baada ya mimba kuharibika, nilipata vizuri ingawa mwanzo nilikuwa na hofu nawaza kwamba itakuaje wasijesema nimetoa mimba, nesi nitakayemkuta naye atanipokea vipi lakini nilivyofika kituo cha afya Katunguru nilipokelewa vizuri kwa kweli.”

Hao ni wachache wanaowakilisha wengi wasiojua kuwa, matumizi ya uzazi wa mpango husaidia kupunguza vifo vya wajawazito kwa takriban asilimia 40 kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa.

Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto Mkoa wa Mwanza, Cecilia Mrema katika mazungumzo na HabariLEO anasema kuwa, mama anapokuwa na utaratibu wa kuzaa kwa mpango huimarisha afya yake kabla ya kubeba ujauzito mwingine.

Kwa mujibu wa Cecilia, Mkoa wa Mwanza una asilimia 24 ya uhitaji wa uzazi wa mpango, lakini wengi hawafiki huduma hizo kutokana na changamoto ya maeneo ikiwemo visiwani.

“Wengi wanahitaji uzazi wa mpango, lakini changamoto ni ufikiwaji, hata hivyo tunajitahidi kuwafuata huko huko visiwani,” amesema na kuongeza kuwa, lengo la afua ya uzazi wa mpango ni kupunguza vifo vya uzazi na watoto wachanga. 

 Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa, wanawake wakitumia sawia njia za uzazi wa mpango, wanaweza kupunguza vifo kwa asilimia 40.

“Asilimia 24 ya wanawake wanahitaji huduma za uzazi wa mpango, lakini hawajazipata; Maria Stopes wanatusaidia kufika kule ambako wengine wanashindwa kufika kupitia Mpango wa Kuimarisha Huduma katika Vituo vya Afya vya Serikalli (PSS),” anasema.

Kwa mujibu wa mratibu huyo,  kwa sasa Mkoa wa Mwanza una vituo 52 vinavyotekeleza mradi wa PSS.

“Vile vituo vimewezeshwa kila kitu, tulikuwa na changamoto ya ujuzi wa kutoa njia za uzazi wa mpango, vifaa na kuwapata akinamama, utakuta mtu yupo kituoni ana kila kitu lakini, akina mama hawapo kwa kuogopa au kutokana na kutokuwa na uelewa,” anasema.

Amesema, kila kituo kilichoingia kwenye mpango huo, watumishi wake wawili wamepewa mafunzo.

“Mtumishi akishafundishwa hana sababu ya kusema siwezi kwa maana kila kitu anakuwa nacho,” anasema.

Ripoti ya Hali ya Idadi ya Watu Duniani ya mwaka 2022, iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, (UNFPA) inasema karibu nusu ya mimba zote takribani milioni 121 kila mwaka duniani kote, hazikutarajiwa.

Ripoti hiyo iliyopewa jina: “Kuona Yasiyoonekana: Kuchukua Hatua Katika Janga Lililopuuzwa la Mimba Zisizotarajiwa,” inaonesha idadi kubwa ya mimba zisizotarajiwa ni matokeo ya kushindwa kutetea haki za msingi za wanawake na wasichana, duniani kote.

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani (WHO) mwaka 2022 lilitoa mwongozo wake kuhusu huduma ya utoaji mimba salama ili kulinda afya ya wanawake na wasichana na kusaidia kuzuia zaidi ya visa milioni 25 vya utoaji mimba usio salama ambao hivi sasa unafanyika kila mwaka.

Faida za Uzazi wa Mpango:

Dk Ritha Chuwa kutoka Maria Stopes anasema uzazi wa mpango  inampunguzia  baba msongo wa mawazo unaotokana na ulezi wa familia isiyopangiliwa.

Pia anataja faida nyingine ni  kuokoa maisha ya mama, watoto wachanga na wasichana, hukuza uchumi na maendeleo ya familia, inachangia kukuza maendeleo ya nchi, hupunguza idadi ya mimba zisizotarajiwa na kuharibika kwa mimba, huboresha afya ya Mama, baba, watoto wachanga, mwenzi na familia kwa ujumla.

       Nani anaweza kutumia?

Dk Ritha anasema mtu yeyote ambae amepevuka na anaweza kujamiana anaweza kutumia huduma za uzazi wa mpango. 

“Huduma ni mahususi kwa vijana, wanawake, wanaume waliooa, wasioolewa, wenye watoto na ambao bado hawajapata watoto au watu  wenye ulemavu,” anasema. 

Anasema watu wote wana haki ya kupata taarifa sahihi, elimu na huduma ya uzazi wa mpango, bila kujali wana watoto wangapi au hali ya ndoa.

Kuna njia zipi za uzazi wa mpango? 

Kuna aina mbali mbali za njia za uzazi wa mpango ambazo unaweza kuchagua kama zifuatazo; njia za muda mfupi ambazo  ni midonge, sindano, mipira ya kike na kiume na pia njia za asili.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo njia hizi ni nzuri hasa kwa wale watu ambao wanataka kupata mtoto mwingine ndani ya miaka miwili ijayo 

Njia hizi za uzazi wa mpango mwanamke /mwanamume anaweza kupata, kusababisha ujauzito mara anapoacha kutumia.

Baadhi ya njia za muda mfupi hutengeneza kizuizi kinachozuwia mbegu zisikutane na yai.

 Njia za muda mrefu:

 Hizi ni vipandikizi na kitanzi ‘lupu’

Anasema njia hizi pia zinaweza kutumika kwa mwanamke na mara anapoacha kutumia anaweza kupata ujauzito.

Njia hizi ni nzuri hasa kwa wale watu ambao wanataka kupumzika kwa muda mrefu kabla ya kupata ujauzito mwingine, miaka mitatu au zaidi. 

Njia hizi zina ufanisi wa hali ya juu na zinatumika kwa muda mrefu

       Njia za kudumu: 

Hii ni njia ya kufunga uzazi kwa hiari kwa mwanamke au mwanaume

Njia hii ya uzazi wa mpango ni ya kudumu. 

Njia hii ni kwa wale walioamua kutokupata watoto tena

     Mambo ya kuzingatia:

Kuna mambo mengi ya kuzingatia wakati wa kuchagua njia ya uzazi wa mpango kama vile ni  muda gani mtu au wenzi wanataka kusubiri kabla ya kupata ujauzito, unahitajika.

Habari Zifananazo

11 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button