DAR ES SALAAM; Rais mstaafu wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa shindano la Binti Afrika linalotarajia kufanyika Kijichi mkoani Pwani Machi 9 mwaka huu.
Akizungumza na HabariLEO, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya KL International Argency, inayoandaa tukio hilo, Alfonce Mkama amesema maandalizi yote yamekamilika wanasubiri uzinduzi.
“Lengo la shindano la Binti Afrika ni kukuza lugha ya Kiswahili pamoja na maadili ya kiafrika, ambapo vigezo vyote hivyo vitazingatiwa katika kumpata mshindi,” amesema na kuongeza:“Hili ni shindano la mabinti wenye shepu zao za kiafrika, maana wengine wanalifananisha shindano hili na mashindano mengine ya warembo ambayo huwakilishwa na warembo wembamba.’
“Naomba wananchi wajiandae kushuhudia shindano letu linalotarajiwa kuleta mageuzi makubwa na kutoa ajira na kubadilisha maisha ya mabinti hao,” amesema Mkama
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kingazi Resort, ambako ndiko warembo hao wanafanya mazoezi na litakapofanyika tukio hilo, Yerikoe Mahenge amesema mabinti hao wanaendelea na mazoezi katika eneo hilo ambalo lina utulivu wa aina yake.