DODOMA; SERIKALI ina mpango wa kujenga uzio wa umeme wa majaribio katika eneo la Kilometa 68 Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Maelezo hayo yametolewa bungeni leo Juni 4, 2024 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Aleksia Kamguna aliyetaka kujua lini Serikali itajenga uzio wa umeme katika Hifadhi ya Mikumi, ili kuepusha usumbufu wanaoupata wananchi wanaopakana na hifadhi hiyo kutoka kwa wanyama.
“Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ina mpango wa kujenga uzio wa umeme wa majaribio katika eneo la kilometa 68 katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa maeneo yanayopakana na vijiji vya Wilaya ya Serengeti na Tarime.
“Kwa sasa Wizara ipo kwenye majadiliano na wadau wa maendeleo kwa lengo la kupata fedha.
“Aidha, endapo uzio huo utaonesha ufanisi, Serikali itaendelea kujenga uzio kama huo katika maeneo mengine yenye changamoto kubwa ya wanyamapori wakali na waharibifu ikiwemo Hifadhi ya Taifa Mikumi kulingana na upatikaji wa Fedha,” amesema Naibu Waziri.
Pia amesema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo pindi wanapoingia kwenye maeneo ya wananchi.
“Hatua hizo ni pamoja na kutumia helikopta, magari maalum, ndege nyuki (drones), matumizi ya mabomu baridi na doria za kawaida.
“Sambamba na hatua hizo, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu,” amesema.