MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Kampasi ya Moshi, imebuni mashine maalumu ya kukandamiza kwa ajli ya kukata na kukunja vyuma vya kutengenezea bidhaa mbali mbali ikiwemo vijiko, makofuli, komeo za milango na mageti, nati, bawaba za madirisha, umma na bidhaa nyingine za aina hiyo.
Hayo yamebainishwa leo Julai 2,2023 na mwanafunzi wa mwaka wa pili wa chuo hicho, Petro Daudi katika banda la taasisi hiyo kwenye Maonesho ya Biashara ya 47 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DTIF) yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba.
Amesema, kumekuwa na uhitaji mkubwa wa mashine hiyo ambayo inarahisisha uzalishaji wa bidhaa kwa wingi.
“Mashine hii ni maalum kwa ajili ya kukata, kutoboa, kukunja, kutokana na vifaa vya uzalishaji vyenyewe vilivyofungwa, na imekuwa mkombozi kwa wazalishaji wa bidhaa za chuma.”Amesema
Nae, mwalimu Irene Muro wa chuo hicho anasema VETA imekuwa ikibuni teknolojia mbali mbali kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi ili wakimaliza masomo yao wapate ujuzi wa kujiajiri wenyewe.
“Vijana wanachangamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa ajira hivyo mashine hii imetoa ufumbuzi wa ajira kwa sababu mwanafunzi ataweza kutengeneza mashine yake mwenyewe kama hii na atafanya shughuli zake.”Amesema Muro na kuongeza
“Lakini vile vile malighafi zinazotengeneza mashine hii zinapatikana hapa hapa nyumbani na hivyo inatoa unafuu wa gharama kwa wanunuaji.”Amesema
Amesema, mashine hiyo awali ilikuwa zinaagizwa nje kwa gharama ya sh milioni 13 lakini kwa sasa inapatikana hapa hapa nchini kwa gharama ya sh milioni 3.5