Viashiria vya mimba na ndoa za utotoni Rukwa vyapungua

SHIRIKA la Plan International limesema viashiria vinavyowaweka watoto wa kike katika hatari ya kuozwa au kupata mimba wakiwa chini ya miaka 18 vimeanza kupungua kwa kasi inayoridhisha mkoani Rukwa.

Viashiria hivyo ni pamoja na umasikini, elimu duni, shinikizo rika, uelewa mdogo wa jamii kuhusu sheria zinazosimamia masuala ya mahusiano ya watoto na wanafunzi, ukatili na usawa wa kijinsia na idadi ndogo ya shule za bweni na zinazotoa chakula.

Vingine ni malezi hafifu, mila desturi na imani zinazomkandamiza mtoto wa kike, kuporomoka kwa maadili katika jamii, na kutokuwajibika kwa wazazi na viongozi katika ulinzi wa watoto wa kike.

Meneja wa Mradi wa Kupinga Mimba na Ndoa za Utotoni kupitia shirika hilo linalofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Norway (Norad), Kisasu Sikalwanda anasema; “Tulikuja Rukwa kusaidiana na serikali kukabiliana na tatizo hilo na wakati tukianza kutekeleza mradi huu hali ilikuwa mbaya.”

 

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Donald Nsoko anasema kwa takwimu za utafiti wa kidemografia za mwaka 2015 hadi 2016 zinaonesha asilimia 29 ya wanawake wenye miaka kati ya 15 na 19 mkoani humo walikuwa wajawazito au wamezaa.

Kwa mujibu wa utafiti huo, anasema takwimu za matukio ya mimba za utotoni katika mkoa huo zinaonesha katika kipindi cha 2017 hadi 2019 jumla ya matukio 722 ya wanafunzi kupata mimba yaliripotiwa ambayo kati yake 171 yalitokea katika shule za msingi na 551 kwa shule za sekondari.

“Ndipo mwaka 2020 mkoa ukaja na mkakati maalumu wa miaka mitano 2020 hadi 2025 wa kukabiliana na tatizo la mimba na ndoa za utotoni kwa kushirikiana na wadau wake mbalimbali wa maendeleo ikiwemo Plan International,” anasema.

Kwa kushirikiana na Shirika la Yes Tz, Rafiki SDO, Lusudeo, PDF na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Chala, Sikalwanda anasema Plan International inatekeleza afua tano zinazolenga kuusaidia mkoa huo kuhakikisha ifikapo mwaka 2025, tatizo la mimba na ndoa za utotoni linakuwa historia.

Anataja moja ya afua hizo kuwa ni ile inayolenga kuhakikisha mtoto wa kike anakwenda shule kwasababu; “Shule inasadia kumzuia na vishawishi vya mimba au ndoa kwasababu ya sharia, miongozo yake na mikataba mbalimbali ya kimataifa.

Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inayolenga kuimarisha ulinzi, matunzo na haki za mtoto na sheria ya elimu ya mwaka 2016 inayoeleza elimu ya msingi ni ya lazima kwa watoto wote na itatolewa bure.

Nyingine ni sheria ya adhabu ya makosa ya jinai namba 16 inayolinda haki za wanawake na mtoto kwa kuweka adhabu kali kwa makosa ya kujamiiana kama ukeketaji, ubakaji na udhalilishaji.

Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto, Mkataba wa Afrika Kuhusu Haki na Ustawi wa Mtoto na Sera ya Maendeleo ya Mtoto.

Miaka mitatu baada ya mradi huo kutekelezwa, anasema tafiti zinaonesha utoro wa wanafunzi wa kike ukiwemo ule unaosababishwa na masuala yanayohusiana na hedhi unapungua huku; “Taarifa za mimba na ndoa za utotoni nazo zikipungua.”

Katika shule ya Msingi Itindi wilayani Nkasi, mwalimu wa Malezi, Lilian Ega anasema elimu ya hedhi salama na mpango wa kugawa taulo za kike kwa wanafunzi umesaidia kupunguza utoro kwa zaidi ya asilimia 50.

“Utoro kwa watoto wa kike utapungua zaidi endapo shule itaanza kupata mahitaji kamili ya taulo za kike. Hivi sasa tunapata pakiti tatu wakati mahitaji ni pakiti 20 hadi 30 kwa mwezi ambayo kati ya wanafunzi wake 750, wanafunzi 460 ni wa kike,” anasema Mwalimu Ega.

Akizungumzia kiashiria cha ufaulu, mwalimu huyo anatoa mfano akisema kati ya wanafunzi wa kike 39 waliomaliza darasa la saba mwaka 2015 ni mmoja tu ndiye alifaulu kwenda sekondari tofauti ni wanafunzi 43 kati ya 56 waliofaulu mwaka jana ikiwa ni matokeo ya utekelezaji wa mradi huo.

Kwa upande wa mafanikio ya kukabiliana na mimba za utotoni anasema Januari mwaka huu alibainika mwanafunzi mmoja kuwa na ujauzito hiyo ikiwa ni toka wanafunzi watatu wabainike mwaka 2017.

Mwalimu Ega anasema baada ya kujengewa uwezo kila Ijumaa ya wiki ni siku ya kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu mimba na ndoa za utotoni, madhara yake, visababishi na namna ya kujiepusha nayo.

Plan International inawapongeza walimu wote katika maeneo ya mradi ikisema wameusaidia mkoa kufikia mafanikio hayo kwani kwa kupitia afua ya elimu ya afya ya uzazi wamewezeshwa kutoa elimu ya moja kwa moja kwa wanafunzi ili wajiepusha na mimba na ndoa za utotoni.

“Kwa kupitia afua hii wanafundishwa kuhusu stadi za maisha, mabadiliko ya mwili katika kipindi cha balee, jinsi na ujinsia, via vya uzazi, mimba na ndoa za utotoni pamoja na njia zake za kujiepusha, ukatili wa kijinsia na magonjwa ya ngono,” anasema.

Mratibu wa shirika la Yes Tz, Shabani Ramadhani anatolea mfano wa shule ya Sekondari Vuma ya Sumbawanga Vijijini ambayo wakati mradi huo ukianza mwaka 2020 iliripotiwa kuwa na wanafunzi sita wenye mimba lakini baada ya hapo haijawahi kuwa na tukio lolote.

“Mradi unawafikia vijana wa rika balee wa kati ya miaka 10 na 24 ndani na nje ya shule katika wilaya ya Nkasi, Kalembo na Sumbawanga Vijijini,” anasema Shabani.

Mmoja wa wanafunzi wa darasa la sita katika shule ya Msingi Itindi, Lidia Wampembe (15) anasema pamoja na kutembea umbali mrefu kutoka nyumbani hadi shule ameweza kukabiliana na changamoto zinazotaka kumuhatarisha na mimba na ndoa za utotoni.

“Natumia dakika 20 kutoka nyumbani hadi shule. Njiani nakutana na wavulana kwa wanaume wanaoniita ovyoovyo na kunitishia. Lakini nimekuwa nikiwaripoti kwa uongozi wa shule ambao naamini umekuwa ukichukua hatua,” anasema.

Anasema hiyo ni baada ya kufundishwa masuala yanayohusu ukatili wa kijinsia na madhara ya mimba na ndoa za utotoni na namna ya kujilinda kimwili na kiafya na kujiepusha na makundi hatarishi.

Mtendaji wa kijiji hicho cha Itindi, Charles Nkungu anasema ulinzi na usalama wa mtoto ni wajibu wa kila mtu na wao kama kijiji wamekuwa wakishirikiana na wadau mbalimbali kuelimisha jamii juu ya haki, ustawi wa mtoto na wajibu wa mzazi au mlezi katika kumlea na kumlinda mtoto.

“Serikali ya kijiji kwa kushirikiana na wazazi, walezi au walimu tumeweka utaratibu unaotuwezesha kujua kama watoto wanakwenda shule na kurudi nyumbani kwa wakati. Hiyo ni baada ya kupokea malalamiko kwamba baadhi ya wanafunzi hawafiki shule na hawarudi nyumbani kwa wakati” anasema.

Katika kijiji hicho, Nkungu anasema wameunda pia kamati ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (Mtakuwa) inayoshughulikia matukio ya ukatili kwa makundi hayo na kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuripoti katika vyombo vya dola.

Matokeo ya utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Masuala ya Afya ya Uzazi (UNFPA) uliotolewa Julai mwaka jana unaonesha karibu theluthi moja ya wanawake wote katika nchi zinazoendelea wanaanza kupata watoto wakiwa na miaka 19 au chini ya hapo na karibu nusu ya uzazi wote wa mara ya kwanza huwa ni wa watoto au wasichana wa chini ya miaka 18.

Wasichana wanaoolewa wakiwa wadogo hawapati fursa za elimu na kiuchumi ambazo zinasaidia kuwatoa katika umasikini ambavyo ni muhimu kwa ajili kujenga mustakabali endelevu na wenye mafanikio kwa ajili yao, jamii na Taifa

Habari Zifananazo

Back to top button