Vifaa tiba kukabiliana na kipindupindu Kanda ya Ziwa

SERIKALI imetoa vifaa tiba na kinga vyenye thamani zaidi ya Sh milioni 7 kwenye mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu pamoja na dawa za kutibu maji kwa kuua wadudu wenye vimelea vya ugonjwa huo.

Hayo yalisemwa Januari 24, 2023 na mganga mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu alipofanya ziara wilayani Kishapu katika kijiji cha Idukilo akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme.

Profesa Nagu alisema wametoa vifaa tiba na kinga kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo imebainika na uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwa wananchi.

Advertisement

“Serikali haina upungufu wa vifaa tiba na dawa tumegawa vifaa tiba na maji yenye dawa kwa watumishi wanao hudumia wagonjwa waliobainika na ugonjwa wa kipindupindu na tumesisitiza suala la usafi na Mazingira kwa wananchi”alisema Nagu.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme alisema eneo hilo limebainika kuwa na ugonjwa wa kipindupindu sababu Kaya 142 zimekutwa hazina vyoo.

“Mmenisikitisha kweli nilipouliza nakuomba taarifa nikajibiwa kaya zina vyoo tulipofanya uchunguzi mdogo kwa haraka tukabaini Kaya 142 hazina vyoo ni aibu kujisaidia vichakani”alisema Mndeme.

Mndeme alisema kwanini wananchi wanashindwa kuchimba vyoo kwenye Kaya zao na kwenda kujisaidia vichakani hali iliyosababisha uchafu wote kwenda mto Tungu ambapo wananchi wanatumia maji hayo kwa kunywa.

“Kijiji cha Idukilo kimeonekana kuwa chanzo cha uwepo wa ugonjwa wa kipindupindu kwa wilaya ya Kishapu nakufanya jumla ya watu wote kwa Mkoa wa Shinyanga waliougua kipindupindu kufikia 139 na waliofariki ni watu sita”alisema Mndeme.

Meneja wa Wakala wa Maji na Mazingira Vijijini (Ruwasa) Mhandisi Dickson Kamazima alisema wananchi wa kijiji hicho walikuwa wanautumia mto Tungu kupata maji baada ya jenereta kuharibika kusukuma maji ambapo kisima kilichopo kijijini hapo kina urefu wa mita 130 na ujazo Lita 12,0000 na uwezo wa kuhudumia wananchi zaidi ya 4000.