Vifo mapigano Sudan vyafikia 200

WATU 200 wameuawa na wengine 1,800 kujeruhiwa katika siku tatu za mapigano kati ya ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) tangu kuanza kwa mapigano hayo mwishoni mwa wiki iliyopita nchini Sudan.

Kwa mujibu wa mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Volker Perthes ametoa wito kusitishwa kwa mapigano hayo haraka iwezekanavyo, huku akitaka vikosi hivyo kumaliza mzozo uliopo.

Imeelezwa kuwa pande hizo mbili zinatumia vifaru, mizinga na silaha nyingine nzito katika maeneo yenye watu wengi hata hivyo ndege za kivita zilinguruma na moto kusambaa angani nyakati za usiku.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York kupitia video, Perthes pia alisema kwamba pande zinazozozana “hazitoi hisia kwamba zinataka upatanishi wa amani kati yao”.

Mwishoni mwa wiki iliyopita mataifa ya Marekani, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zilitaka pande hizo mbili kuzima uhasama mara moja bila masharti.

Awali taarifa ya jeshi la Sudan ilisema kuwa wanajeshi wake walikuwa kifua mbele kwenye vituo vya RSF huko Khartoum na majimbo mengine.

Taarifa hiyo ilifafanua wanajeshi walidhibiti kambi za Omdurman, mji pacha wa Khartoum katika Mto White Nile, na kuongeza kuwa jeshi litamaliza mzozo huo hivi karibuni.

Aidh, RSF ilikanusha taarifa ya vikosi vya jeshi, ikisisitiza kuwa mapigano yalikuwa yanaendelea. Kundi hilo la kijeshi lilidai zaidi katika taarifa kwamba vikosi vyake viliangusha ndege ya kijeshi siku ya Jumamosi usiku.

Watu walioshuhudia mjini Khartoum walisema kwamba mamia ya watu, wakiwemo zaidi ya watoto 400 wa shule, walizuiliwa katikati mwa jiji la Khartoum, ambako mapigano makali yalikuwa yakitokea karibu na makao makuu ya jeshi.

Habari Zifananazo

Back to top button