Vifo mapigano Sudan vyafikia 56

IDADI ya vifo katika mapigano yanayoendelea kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) imefikia 56 huku waliojeruhiwa ni 595, Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan ilisema katika taarifa yao leo Aprili 16, 2023.

Kamati hiyo imetoa wito kwa Jeshi la ‘RSF’ na Jeshi la Sudan kuanza mazungumzo ya amani ili kuwezesha uokoaji wa waliojeruhiwa, haswa miongoni mwa raia.

“Tunatoa wito kwa vikosi vyote kufungua njia salama kutoka kwa wagonjwa walio katika kituo cha kusafisha damu karibu na kamandi ya jeshi huko Khartoum,” ilisema taarifa hiyo.

Wakati huo huo, mapigano kati ya pande hizo mbili yaliendelea kwa siku ya pili mfululizo katika maeneo tofauti ya mji mkuu Khartoum, hasa katika au karibu na makao makuu ya jeshi.

Milio ya risasi na milio mikubwa ya risasi inasikika katika mji Mkuu wa Sudan, Khartoum, kwa siku ya pili.

Mapigano hayo yanameendelea leo huku Marekani, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zikitaka pande hizo mbili kuzima uhasama mara moja bila masharti.

Taarifa ya jeshi la Sudan imeeleza kuwa wanajeshi wake walikuwa kifua mbele kwenye vituo vya RSF huko Khartoum na majimbo mengine.

Taarifa hiyo ilifafanua wanajeshi walidhibiti kambi za Omdurman, mji pacha wa Khartoum katika Mto White Nile, na kuongeza kuwa jeshi litamaliza mzozo huo hivi karibuni.

RSF imekanusha taarifa ya vikosi vya jeshi, ikisisitiza kuwa mapigano yalikuwa yanaendelea. Kundi hilo la kijeshi lilidai zaidi katika taarifa kwamba vikosi vyake viliangusha ndege ya kijeshi jana usiku.

Watu walioshuhudia mjini Khartoum walisema kwamba mamia ya watu, wakiwemo zaidi ya watoto 400 wa shule, walizuiliwa katikati mwa jiji la Khartoum, ambako mapigano makali yalikuwa yakitokea karibu na makao makuu ya jeshi.

Pia, Umoja wa Mataifa ulisema wafanyakazi watatu wa kutoa misaada waliuawa huko Kabkabiya Darfur Kaskazini.

Habari Zifananazo

Back to top button