Vifo shambulio la kigaidi Moscow vyafikia 115

MOSCOW, Russia: KAMATI ya Uchunguzi ya Urusi imetangaza kuwa idadi ya watu waliouawa kutokana na shambulio la kigaidi kwenye jumba la tamasha la Moscow ‘Crocus City Hall’ imeongezeka kufikia watu 115.

Idadi hiyo inajumuisha watoto watatu kama ilivyoripotiwa na jarida la serikali ya Urusi TASS.

TASS ilinukuu Idara ya Usalama ya Shirikisho (FSB) ikisema kuwa watu 11 wamezuiliwa, wakiwemo magaidi wanne waliohusika katika shambulio hilo.

Advertisement

Washukiwa hao wanadaiwa kujaribu kutoroka kuelekea mpaka wa Urusi na Ukrain.

“Magaidi walipanga kuvuka mpaka na walikuwa na mawasiliano upande wa Ukraine,” ujumbe huo ulisomeka.

Kituo cha Telegram cha Urusi cha Baza kiliripoti madai ya kuhusika kwa raia kutoka Tajikistan katika shambulio hilo, huku picha za wanaodaiwa kuwa washukiwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii.