WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imesema vifo vya watu watatu vilivyotokea katika kata ya Kisale Msaranga , wilayani Rombo , mkoani Kilimanjaro havina uhusiano wowote na ulaji wa nyama.
Katibu mkuu wa wizara hiyo, Profesa Riziki Shemdoe amesema hayo Mei 23,2023 kwa waandishi wa habari mjini Morogoro baada ya kusaniwa kwa mashirikiano kati ya taasisi 11 zilizochini ya wizara hiyo na Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo (SUA).
Profesa Shemdoe amesema kuwa baada ya kuriporiwa na vyombo vya habari kuwa Watu hao walifariki baada ya kula chakula msibani, timu ya wataalamu wa Kanda ya Kaskazini kupitia vituo vyake vya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) vilifanya uchunguzi na kwamba hapakuwa na mahusiano vifo vyao na nyama waliokula.
“Taarifa tuliyonayo waliyotupati wataalamu wetu ya kwamba vifo vile havina mahusiano yoyote na ulaji wa nyama kama iliyoelezwa”amesema Profesa Shemdoe.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amesema tayari wenzao wa Idara ya Afya wameshachukua sampuli kwa wale wanaojisikia vibaya ili kufanya utaratibu wa kuchunguza kinachoendelea.
Hivi karibuni zili ripotiwa taarifa za watu watatu wakazi wa kata ya Kisale Msaranga, wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, kufariki dunia muda mfupi baada ya kula chakula msibani kutokana na kilichodaiwa ni kuharisha, kutapika, kutokwa na makamasi yenye damu pamoja na kusikia maumivu ya mgongo na kichwa.