HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imeteua wagombea wa nafasi za uongozi wa mikoa wakiwamo wa jumuiya za chama.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Godwin Mkanwa amepitishwa kutetea kiti chake.
Katibu Mkuu wa CCM, Mkoa wa Dodoma, Pili Mbanga akizungumza na HabariLEO jijini Dodoma jana alisema wagombea wengine ni Adam Kimbisa na Augustine Gaulanga.
Katika nafasi ya Mjumbe wa NEC ni pamoja na Ismail Ibrahim, Dayan Ngurumo, Ahid Sinene, Felister Bura, Nicholas Haule na Donald Majitii.
Uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 16 kwa upande wa Umoja wa Vijana, Novemba 17 kwa upande wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Novemba 18, itakuwa ni kwa Jumuiya ya Wazazi wakati uchaguzi kwa nafasi ya Uenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dodoma itakuwa ni Novemba 21, mwaka huu.
Wagombea wa UV-CCM ni pamoja na Jesca Mshana, Abdulhabib Mwanyemba, Yonah Lekele na Jamali Shaban.
Katika nafasi ya Mwenyekiti wa UWT Mkoa, wagombea waliopitishwa ni Neema Majule, Kaundime Kassase, Elizabeth Lameck na Zabibu Mafita.
Katika nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa, majina matatu yaliyopitishwa ni pamoja na Dk Damas Kashegu, Samweli Makasi na Samweli Malecela.
Katibu wa CCM Mkoa wa Geita, Alexandrina Katabi alilieleza HabariLEO jana kuwa makada wanne wamepitishwa kugombea nafasi ya uenyekiti wa CCM Mkoa akiwamo Said Karidushi anayetetea kiti hicho, Daudi Sunzu, Kasendamila Nabaya na Wanselho Siwale.
Katabi alisema nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Taifa (MNEC) waliopitishwa ni Adeline Kabakame, Lameck Mgasha pamoja na Evarist Gervas ambaye anaendelea kutetea kiti hicho.
Alisema wagombea waliopitishwa nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa ni Hamis Kajole, Sospeter Burugu, Manjale Magambo na Richard Juba ambaye ni mtetezi wa nafasi hiyo.
Katabi alisema nafasi ya uenyekiti wa UWT ni Safia Bakari akiwa ni mtetezi wa nafasi hiyo na wengine ni Lorensia Bukwimba aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Busanda na Mariam Warwa.
Pia katika nafasi ya Jumuiya ya Wazazi waliopitishwa kugombea nafasi ya uenyekiti wa jumuiya mkoa ni Lucas Mazinzi anayetetea nafasi hiyo, Mary Mpangalala na Masclej Chula.