Vigogo Chadema waliomkataa Mwenyekiti Katavi wabanwa
UONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilaya ya Mpanda, umewataka viongozi wa jumuiya za chama hicho wilayani humo, kuomba radhi kwa madai ya kutoa kauli zilizozua taharuki ndani ya chama.
Viongozi hao ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema(Bavicha) Wilaya ya Mpanda, Elizabeth Kasera na Katibu Baraza la Wanawake (Bawacha), Wilaya ya Mpanda (BAWACHA), Hamisa Korongo, ambao inadaiwa walitoa taarifa kwenye vyombo vya habari ya kumkataa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Katavi, Rhoda Kunchela.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za chama hicho, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chadema, Wilaya ya Mpanda, Khalfan Zozi, amesema baada ya vikao kadhaa, wamekubaliana kuwa viongozi hao wasamehewe, lakini sharti ni kuomba msamaha kwa wanachama, kupitia vyombo vya habari, ili kuondoa taharuki waliyoizusha kwa wananchi.
Viongozi hao inadaiwa walisema Mwenyekiti wao amekitelekeza chama chao baada ya uchaguzi wa mwaka 2020, ikiwa ni pamoja na kuchukua baadhi ya vitu vya ofisi kwa maelezo vilikuwa vya kwake binafsi.
Walidai kuwa wanamtambua Almasi Ntije kwamba ndiye Mwenyekiti wao, kwani wamekuwa naye katika kukipambania chama.
Kwa mujibu wa Zozi, Mwenuekiti Kunchela aliondoka mkoani humo, baada ya kuhisiwa usalama wake ni mdogo, hivyo akawa mafichoni kwa muda na si kwamba alikitelekeza chama.
“Baada ya uchaguzi, kulikuwa na baadhi ya taarifa ambazo sio salama sana kwa aliyekuwa mgombea wetu, ambaye vilevile ndio Mwenyekiti wa chama wa mkoa, kwa ajili ya usalama wake ilibidi aondoke Mpanda na kitendo cha yeye kutokuwepo wakawa wamekaimishwa viongozi wengine,” alisema.
Amesema Kunchela aliondoka kwa kufuata taratibu zote, hivyo anapaswa kuheshimiwa kwa kuwa bado ni Mwenyekiti wa chama hicho hadi sasa.