Vijana EAC wafundishwa kuhusu amani

SHIRIKA lisilo la kiserikali Agrithaman, limetoa mafunzo kwa vijana 30 wanaotoka katika mashirika mbalimbali mkoani Kagera kuhusu nafasi ya vijana kudumisha amani na kujiepusha na migogoro inayowakumba wanaposaka fursa za kiuchumi katika mikoa inayopakana na Maziwa Makuu.
Nchi nyingine zilizo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambazo vijana wake wanashiriki mafunzo kama hayo mbali na Tanzania ni Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda na Burundi.
Meneja wa Agrithaman, Mwasiti Kazinja aliitaja mikoa mingine ya Tanzania iliyo katika mradi huo wa Mtandao wa Vijana wa Nchi za Maziwa Makuu kwa Maelewano na Amani Mradi unaodhaminiwa na taasisi ya Konrad Adenauer Stiftung (KAS) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) ni Kigoma, Geita na Mwanza.
Kwa mujibu wa Kazinja, mafunzo hayo yanalenga kuwafanya vijana wawe chachu na washiriki kikamilifu katika juhudi za kudumisha amani na utulivu katika mikoa iliyopo pembezoni mwa maziwa makuu.
Naye Mratibu wa mradi nchini Tanzania, Jimmy Luhende, aliliambia HabariLEO Afrika Mashariki kuwa, mradi huo ulianza mwaka 2021 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2024.
“Katika awamu ya kwanza ya mradi, vijana 25 walipata mafunzo kuhusu namna wanavyoweza kudumisha amani na utulivu nchini Tanzania na kuanzisha mitandao na mijadala baina yao na vijana wa nchi nyingine,” alisema Luhende.
Akaongeza: “Jambo kubwa walilojifunza ni jukumu walilo nalo katika kuimarisha amani na namna wanavyoweza kushirikiana na taasisi za serikali, na wadau wengine kuendeleza ajenda ya amani na utulivu katika nchi zao.”
Luhende alisema kila mwaka vijana zaidi ya 100 hukutanishwa katika nchi mojawapo sambamba na sherehe za maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana katika Tamasha la Shule ya Amani na Utulivu.
Mwaka 2021 vijana hao walikutana Goma nchini DRC wakati mwaka jana, walikutana nchini Uganda. Kwa mwaka huu, Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano huo. Kwa sasa makao makuu ya mradi yapo DRC.