WAKATI wa maonesho ya wakulima na wafugaji, maarufu Nanenane yaliyofanyika kitaifa jijini Mbeya, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliwataka vijana nchini hususani wasomi, wasihofu kuingia kwenye kilimo kwani kinalipa tofauti na wengi wanavyofikiri.
Waziri Mkuu Majaliwa alitoa wito huo wakati akizindua Mpango Maalumu wa Kuwawezesha Vijana kuingia kwenye Kilimo uliobuniwa na Wizara ya Kilimo unaojulikana kama ‘Building a Better Tomorrow (BBT)’.
Amesema vijana wanapaswa kugeukia kilimo na hasa kwa kuzingatia mikakati ya serikali iliyopo ikihusisha kuongezwa kwa bajeti ya kilimo kutoka Sh bilioni 276.6 hadi bilioni 926.
Waziri Mkuu Majaliwa amewataka vijana wasihofu kungia kwenye kilimo kwa sababu kina manufaa makubwa. Wala wasiache kuingia kwa kuhofu kupata mitaji kwa sababu serikali imetoa maelekezo kwenye benki zote kukopesha wajasiriamali wanaojishughulisha na kilimo wakiwemo vijana.
Amesema mikopo pia inapatikana kwenye halmashauri zao ambako wanapaswa kwenda kuomba na kwamba kinachotakiwa kwao ni kuandika mpango-kazi.
Kauli ya waziri Mkuu Majaliwa inaonesha utashi wa serikali katika kuboresha kilimo na kwa hatua hiyo shughuli za utafiti wa kilimo, mifugo na uvuvi zinaongezeka maradufu pamoja na uzalishaji mbegu.
Bajeti inawezesha utayarishaji wa maeneo mengi zaidi ya kilimo cha umwagiliaji, kuanzisha mashamba makubwa yanayowekewa miundombinu muhinu kwa ajili ya kilimo (block farming) ambayo yatagawiwa kwa vijana, kuongeza maofisa ugani na mengine mengi.
Tukizungumzia mashamba makubwa kwa mfano, yatawanyanyua zaidi kuliko wanapokuwa wakilima mmoja mmoja kwa kuwa mashamba makubwa yatakuwa na miundombinu muhimu, rahisi kupeleka utalaamu na pia kutakuwa na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na hivyo kuwahakikishia soko.
Tunaungana na Waziri Mkuu Majaliwa kuwahimiza vijana ambao ndio idadi kubwa ya Watanzania kuchangamkia kilimo na kuondoa fikra kwamba ukishasoma basi shughuli inayokufaa ni kukaa ofisini na mafaili.
Kwamba vijana hawana sababu ya kukimbilia mijini wakidhani kilimo ni kazi ya wazee bali wajue kilimo ni kazi yenye manufaa makubwa kama nyingine na hasa endapo mtu atalima kisasa.
Tunaamini vijana wengi watakapogeukia kilimo nchi itazalisha mamilionea wengi na kumaliza tatizo la ajira.Vijana wanatakiwa pia kuunda vikundi ili iwe rahisi kukopesheka na hata kudhibitiana kurejesha mikopo.
Tunaishauri serikali kuendelea kuhimiza vijana wawe na mwamko wa kilimo kwa kuwaandaa vyema huku ikiendelea kuwekeza ili maizngira yazidi kuwa rafiki katika mnyororo wa kilimo.
Waswahili wanasema jembe halimtupi mkulima lakini vijana wajue pia kwamba serikali imesimama sawia kwenye mtazamo wa mzazi aliyewaambia wanawe kwenye shairi moja maarufu kwamba: “Kama mnataka mali mtaipata shambani.”