Vijana kufundwa masuala ya uongozi
Anastazia Anyimike, DodomaAugust 2, 2023

VIJANA 1,000 nchini wanatarajia kushiriki kongamano la maendeleo ya vijana linalolenga kujadili masuala ya uongozi na utawala bora ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Akizungumzia jijini Dodoma,Ofisa Maendeleo ya Vijana Mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Amina Sanga, amesema kongamano hilo la siku mbili, vijana watapata fursa za kufahamu masuala yao na ni utekelezaji wa sera ya vijana.

“Sera ya vijana inatutaka tuwakutanishe vijana kwa ajili ya makongamano ya kuzungumzia fursa na masuala yanayotekelezwa na serikali, watajifunza kutoka kwa vijana wengine wa ndani na nje ya nchi,”alisema.
Alisema serikali inaunga mkono makongamano hayo na kuwahamasisha vijana kushiriki kwa wingi kwa kuwa ni fursa muhimu kwao.
Awali, Mkurugenzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Vijana Dodoma (DOYODO), Rajab Nonga, alisema kongamano hilo pia litashirikisha vijana kutoka nchi za Afrika Mashariki.
“Katika kongamano hili kuna uwakilishi wa vijana kutoka makundi mbalimbali kama vile bodaboda, wajasiriamali, watu wenye ulemavu na hakuna kijana yeyote atakayeachwa nyuma kwenye kongamano hili,”alisema.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza kuwapo na majukwaa ya kuwakutanisha vijana ili kujadili sera, sheria na kutoa maoni yao.
“Tumekuja na mkakati huu wa kuwaleta vijana pamoja na kongamano limeshirikisha mashirika 32 na Wizara za kisekta,”alisema.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Freedom House, Daniel Lema, alisema vijana watatoka na maazimio yatakayotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
“Tutajadili masuala ya vijana na uchumi, vijana na uongozi, vijana na utawala bora, fursa za kiuchumi kwa vijana, suala la afya ya akili kwa vijana litajadiliwa ambalo limekuwa ni changamoto inawakabili vijana kwasasa.”
“Tutajadili kuhusu vijana na upatikanaji wa rasilimali fedha kupitia fursa zilizopo kama mfuko wa maendeleo ya vijana, mikopo ya halmashauri na asilimia ile inayotengwa kwenye ununuzi wa umma,”