‘Vijana muitikio wao mdogo nyumba za ibada’

ARUSHA: MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ametoa wito kwa wazazi na walezi kutambua jukumu walilonalo la malezi ya kimaadili kwa vijana ili kukabiliana na changamoto ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

Makamu wa Rais ametoa wito huo aliposhiriki Ibada ya kuwekwa Wakfu na Kuingizwa kazini kwa Askofu Mteule Dk Abel Godson Mollel na msaidizi wake Mchungaji Lareiton Lukumay iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati Usharika wa Kimandolu mkoani Arusha.

Amesema pamoja na Tanzania kuwa na idadi kubwa ya vijana bado muitikio wa vijana hao katika nyumba za ibada ni mdogo hali inayopelekea kukosa mafundisho ya dini ambayo yangewawezesha kuwa na maadili na matumizi bora ya mitandao ya kijamii.

Aidha Makamu wa Rais amesema Serikali inayoongozwa na Dk Samia Suluhu Hassan wakati wote itasimamia na kulinda katiba ya nchi ikiwemo haki ya kuabudu kwa wananchi wote bila ubaguzi. Amesema serikali itahakikisha wananchi wanaendelea kuishi kwa amani na kupata huduma bora za kijamii pamoja na kuwekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta zote ambayo ikikamililika itachangia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi wa Taifa.

Makamu wa Rais amewasihi viongozi wote wa dini nchini kusaidia kutoa hamasa kwa wananchi ili wajitokeze kwa wingi kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu. Amesema Serikali inaahidi kufanya jitihada za kuweka mazingira ya haki na wezeshi ili wananchi waweze kushiriki kuchagua viongozi wanaowataka kwa amani na utulivu.

Halikadhalika amesema Serikali inajivunia ushirikiano mzuri uliopo kati yake na taasisi za dini ambao umedumu kwa muda mrefu katika nyanja mbalimbali na inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Kanisa katika utoaji wa huduma za jamii, hususan elimu, afya na maji. Ameiagiza Wizara ya Afya kuhakikisha inatatua changamoto zinazokwamisha ubia baina ya serikali na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center haraka iwezekavyo.

Makamu wa Rais amewapongeza Askofu Dk Abel Godson Mollel na Msaidizi wake Mch. Lareiton Lukumay kwa kuwekwa wakfu na kuingizwa kazini na kuwasihi waamini wa Dayosisi hiyo na Wakristo wote kwa ujumla kutambua wajibu waliyonao kwa Viongozi wa kiroho. Amewaasa waamini kumpa ushirikiano wa dhati ikiwa ni pamoja na kumpenda, kumtii, kumtia moyo na kumwombea kwa Mwenyezi Mungu Askofu Dk Abel Mollel ili aweze kutenda vema kazi yake.

Kwa upande wake Askofu Dk Abel Mollel amesema Dayosisi hiyo itaendelea kushirikiana vema na serikali katika kutoa huduma za kijamii kama vile elimu na Afya. Ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa ushirikiano na Kanisa ambao umewezesha kufanikisha shughuli mbalimbali ikiwemio kupanda miti zaidi ya laki tatu katika mkoa huo.

Habari Zifananazo

Back to top button