“Vijana na Wanawake pokeeni teknolojia mpya

DAR ES SALAAM: SERIKALI imewataka wanawake hasa vijana kuwa tayari kupokea teknolojia mpya zinazoibuka kwa kasi na kamwe wasikubali kushindwa bali wazitumie kwa ubunifu kutoka ngazi moja hadi nyingine kwa kuwa mabadiliko hayo yanachangia serikali kuboresha sera.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Selestine Kakele amesema hayo leo Dar es Salaam katika mkutano wa saba wa Tehama ulioandaliwa na Tume ya Tehama nchini (ICTC).

Amesema takwimu za dunia zinaonesha idadi ndogo ya wanawake katika kuanzisha kampuni changa za Tehama na kusisitiza wanawake hasa Vijana kuwa na hamasa ya kuanzisha kampuni changa lakini ubunifu huo ujikite kutoa suluhu ya ushiriki wa kundi hilo kwenye Tehama.

Advertisement

Aidha amelitaka kundi hilo kujikita kubuni teknolojia rahisi zenye kusaidia waliopo vijijini waweze kujikwamua na shughuli yaani zisaidie maisha ya watu na kuzitaka taasisi za fedha kutoa ufadhili kwa kampuni changa ili ziimarike na zitoe mchango wake kwa Taifa.

Amesema inaendelea kupitia sera ya Tehama nchini ya mwaka 2016 Ili kuiboresha na iweze kwenda na wakati na kutoa mchango wake kwa maendeleo ya nchi.

Imesema sera hiyo inasimamia nguzo sita ambazo ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya Tehama,usimamizi wa mazingira salama ,utoaji wa elimu kuhusu tehama,ubunifu,uchumi jumuishi wa kidigitali na huduma za fedha.

Amesema kupitia maboresho hayo ya sera katika nguzo ya uchumi wa kidigital lengo ni kupunguza ama kuondoa kabisa pengo la watumiaji na wasiotumia tehama
.
Amesema katika eneo hilo litashughulikia vikwazo kwamba kila mtu ashiriki na afaidike na uchumi wa kidigitali.

Amesema wanawake ni jeshi kubwa wakiamua kwa pamoja wanaweza kupunguza pengo hilo hivyo watimize wajibu wao na kwamba pindi wakutanapo na vikwazo wasikate tamaa bali wasonge mbele.

Awali akizungumza Mkurugenzi Mkuu wa ICTC,Dk Nkundwe Mwasaga amesema kupitia mkutano huo Tehama itatoa elimu kwa umma kuhusu changamoto na mafanikio ya wanawake na Vijana katika tehama, uchumi wa kidigitali lakini pia suala zima la mchango wa akili bandia kwa maendeleo.

 

4 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *