Vijana waathirika zaidi kifafa

CHAMA cha Wataalamu wa Kifafa Tanzania(TEA) kimesema kundi la vijana wenye wastani wa miaka 15 na kuendelea wanaongoza kupata ugonjwa wa kifafa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ajali.

Ajali hasa za bodaboda zimetajwa kuwa chanzo za vijana kupata kifafa baada ya kuumia sehemu za kichwani ( ubongo )na kubaki na kovu ambalo baadae huleta athari kwako.

Akizungumza na habariLEO kuhusu siku ya kifafa Duniani ambayo inaadhimushwa wiki ya pili ya mwezi wa Februari, Daktari Bingwa wa uti wa mgongo na mishipa ya fahamu ,Patience Njenje amesema watu wanaoishi na kifafa ni zaidi ya milioni 60 Duniani na kuna ongezeko la watu 34 hadi 75 kwa kila watu 200000 kwa mwaka.

Advertisement

Amesema Afrika inaasilimia kubwa ya watu wanaoishi na kifafa ambapo ni watu 20 hadi 58 kwa kila watu 1000.

Dk Njenje amefafanua kuwa Tanzania ni moja wapo kati ya nchi zenye watu wagonjwa wengi Afrika mfano vijiji vya Wilaya ya Mahenge inaidadi kubwa hadi 37 kati ya watu 1000 na kina watu zaidi ya milioni moja ambao wanakifafa.

“Wagonjwa wa kifafa nchini wako katika hatari ya kifo mara sita zaidi ambapo zaidi ya asilimia 60 ya vifo vinasababishwa na athari za ugonjwa huo moja kwa moja na zaidi ya asilimia 25 ya wagonjwa wa kifafa wanaulemavu ambao umesababishwa na kuanguka wakati mgonjwa anapopata degedege.

Amebainisha kuwa zaidi ya asilimia 36 ya jamii bado wanaamini kifafa inatokana na nguvu za giza na asilimia 50 wanaamini kuwa unaambukiza huku watoto wenye umri wa kwenda shule asilimia 45 hawapelekwi na asilimia 68 mahudhurio yao hayaridhishi .

“Watoto hawa wenye kifafa wanabaguliwa hawaruhusiwi kucheza na wengine hivyo hufichwa na jamii na asilimia 75 ya wagonjwa huenda kuwaona waganga wa jadi na wengine huenda kwa viongozi wa dini.

Aidha amesema baada ya mgonjwa kuathirika asilimia tano hadi 10 ndio huweza kupata matibabu hospitali hivyo wanachelewa kupata matibabu .

Aidha amefafanua sababu zingine za kifafa kuwa ni homa kali kipindi cha utotoni,minyoo wa nguruwe hasa kwa wale wanaokula nyama zake bila kuiva vizuri,mionyoo kutoka kwa papa,uvimbe kwenye ubongo na upungufu wa kinga.

Dk Njenje amesema endapo mgonjwa atapata hali ya kifafa asishikiliwe anapotikisika na wala asiwekewe kitu chochote mdomoni.

“Alazwe ubavu wa kushoto akimaliza kutikisika na kulazwa sehemu salama na kitu cha muhimu asipande kwenye mti,asipande ghrohilorofani,asiogelee na asiendeshe gari.

Amewaasa jamii kuacha kuwanyanyapaa watu wenye kifafa kwani kila mtu ni mgonjwa mtarajiwa na mtu yoyote anaweza kupata ugonjwa huo.