VIJANA kutoka vyuo vinne nchini, wamesema suala la ajira halitakuwa changamoto kwao, baada ya kupata mafunzo yatakayowawezesha kuanzisha biashara, kuendeleza au kuunda kitu kipya, ambacho kitatatua matatizo yaliyopo katika jamii.
Kwa nyakati tofauti wameelezea hayo, wakati wa kufunga mafunzo ya wiki 10 yaliyoanza Julai mwaka huu, yaliyoandaliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), kupitia program yake ya kuibua vijana wenye vipaji kutoka vyuo vikuu yajulikanayo kama ‘Buni Talent Pool’.
Mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu Ardhi (ARU), anayechukua shahada ya kompyuta, Teddy Micky, amesema amefurahishwa na mafunzo hayo kwa kuwa yamemuwezesha kusimama na kuielezea biashara yake pamoja na kupitia sehemu mbalimbali, zitakazomuwezesha kukamilisha biashara, au kitu anachotaka kukianzisha cha ubunifu.
“Katika programu hii mimi na wenzangu tumeanzisha app inayotumia simu ya kiganjani, ambayo itamsaidia mgonjwa kuwasiliana na daktari na kupata huduma hapo alipo,” amesema.
Naye Ibrahim Lasseko, amesema anaamini kuwa Buni Hub ni sehemu fasaha ya kukuza au kufungua vichwa vya wanafunzi wengi wenye mawazo, wakimaliza shule watapata ajira, lakini kupitia hapo wanapata ufumbuzi wa kibiashara utakaowanufaisha.
Kwa upande wake, Mtaalam wa uhusiano kutoka kumbi ya ubunifu ya Buni iliyopo Costech, amesema vijana 42 wamekamilisha mafunzo ya wiki 10, hivyo anaamini kuwa watakuwa msaada mkubwa kwa jamii kutokana na ubunifu watakaobuni.
Ametaja vyuo walivyotoa vijana hao kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ardhi, Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).