Vijana wanufaika mradi wa bomba la mafuta

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imesema mradi wa bomba la mafuta ghafi kwa upande wa Tanzania umepunguza umaskini kwa kuwapatia vijana ajira na kuwajengea nyumba nzuri ambazo awali kabla ya kuhamishwa hawakuwa nazo.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Japhet Hasunga ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Vwawa amesema hayo leo walipotembelea mradi huo wa kupozea mafuta ghafi uliopo kijiji cha Sojo kata ya Ugusile Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.

Hasunga amesema malengo ya kamati kutembelea mradi huo ni kuona fedha za umma zilizoidhinishwa na Bunge zimetekelezwa ipasavyo na kuendana na thamani ya mradi.

Advertisement

Hasunga amesema katika kuzungukia kiwanda cha kupozea mafuta ghafi amesema wamerizika kwa kuona Ila mahojiano zaidi yatafanyika siku zijazo bungeni.

“Kazi yetu kubwa tumekuja kuona na tumejionea uwekezaji huu imekuwa na tija kiasi gani na umekuja kukabiliana na umasikini kwa watu wetu,”amesema Hasunga.

Hasunga amesema baada ya kamati kuidhinisha fedha hizo utaratibu uliopo Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) unabaki kuwa na hicho la kumulika na kuleta ripoti lakini kilichowafurahisha mpaka sasa ni wananchi kulipwa fidia vizuri za fedha na kujengewa nyumba.

Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC) Musa Makame amesema kiwanda hiki eneo la Sojo kinatumika kama mfumo wa kupozea mafuta ghafi ambapo kimefikia asilimia 61 na Kiko kwenye hatua nzuri.

Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Tukai ameishukuru serikali kubuni mradi huu nakuuleta hapa nchini kwa upande wa wananchi wa kijiji cha Sojo wananchi wamefurahi kwa kulipwa fidia na ulinzi umeimarika zaidi eneo hili.

Msemaji wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kwa Afrika Mashariki (EACOP) GUilaume Mallevary amesema mradi huu uko vizuri na shughuli zote walizozianisha wameanza kuzitekeleza na mitambo imejengwa tayari na mabomba yamewasili kwa wingi.

Ofisa programu ya jamii Editha Ngaiza amesema wamekuwa wakitoa elimu ya usalama barabarani na wametoa huduma za jamii (CSR) kwa kuanza kujenga vyumba vitatu vya madarasa, madawati 110 , meza nane na ujenzi wa Ofisi kwenye Kijiji cha Selemu.

Bomba la mafuta linatokea nchini Uganda Hoima hadi nchini Tanzania Mkoa Tanga Chongoleani likiwa na urefu wa kilomita 1443.