VIKUNDI vya vijana vimetajwa kuongoza kwa kutorejesha fedha za mikopo zinazotolewa na halmashauri.
Akizungumza wakati wa mkutano wa vijana waliopatiwa mafunzo ya ujasiriamali yaliyotolewa na Shirika la Forum For International Corporation (FIC) kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) Ofisa Maendeleo ya Vijana kutoka halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mfungo Manyama aliisema kuwa vikundi vya vijana vinaongoza kwa kutorejesha fedha za mikopo zinazotolewa na halmashauri.
Alisema kuwa katika robo ya mwaka jumla ya Sh bilioni 1.36 zilitengwa kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kiasi cha Sh milioni 600 zilienda kwa vijana.
Alisema kuwa mwaka uliopita Oktoba hadi Desemba vikundi 81 vya vijana Machinga waliopelekwa soko la Machinga complex vilikopeshwa Sh milioni 422.
Álisema kuwa katika makundi matatu yanayokopeshwa na halmashauri wanawake wanarejesha vizuri, lakini changamoto ni kwa vikundi vya vijana na watu wenye ulemavu.
Manyama alisema kuwa kuanzia mwaka 2015 mpaka sasa Sh bilioni 13 ziko kwenye mzunguko kati ya hizo Sh bilioni tano ndizo zimerudi .
“Kundi la vijana na wenye ulemavu ndio wanongoza kwa kutorejesha fedha, hizi fedha ni za mzunguko unapokopa rejesha, ili na wengine wakopeshwe,” álisema.
Álisema kuwa kuanzia Juni mwaka huu vikundi vyote vilivyokopa vitatakiwa viwe vimerejesha fedha bila kufanya hivyo wahusika wote watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Ofisa Mawasiliano na ufuatiliaji miradi kutoka shirika la FIC, Irene Mitema Álisema kuwa kwa kushirikiana na Shirika la msaada la Kijerumani (GIZ) chini ya programu ya Mradi wa kukuza ajira na ujuzi kwa vijana Tanzania (E4D) na wadau wengine Kama Ofisi ya Waziri Mkuu Shirika la Maendeleo la Korea (KOIKA), Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD) na umoja wa Ulaya (EU)kwa pamoja wanatekeleza mradi wa ajira kwa vijana, lengo ni kuhakikisha vijana wa Tanzania wanapata fursa na uzoefu na kujifunza kupitia vijana wenzao waliofanikiwa.
Ofisa Maendeleo ya biashara kutoka Sido, Crispine Kapinga alisema kuwa lengo ni kuhakikisha vijana wanapata uhalisia zaidi wa kile walichojifunza ili kilete tija.
MRADI wa kukuza ajira na ujuzi kwa vijana Tanzania (E4D) unatoa mafunzo ya namna ya kupata zabuni katika miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na kampuni za nje ya nchi, lengo likiwa ni kuwezesha watanzania kushiriki na kushinda.
Vijana waliopatiwa mafunzo hayo waliishukuru serikali na wadau kwa kutoa fursa za mafunzo kwa vijana, kwani wameweza kujiajiri na kutoa ajira kwa vijana wengine.