VIJANA wametakiwa kuchangamkia fursa za mikopo bila riba inayotolewa katika Halmashauri zote nchini, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na ukosefu wa ajira.
Akizungumza katika mahafali ya mafunzo ya Matumizi ya Programu ya kidigitali kwa vijana yanayotolewa na taasisi isiyo ya Kiserikali ya Camara Education Tanzania, Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Temeke, Regina Chami, amesema ni vyema vijana wakatumia mitandao ya kidigitali kwa manufaa ya kujiajiri.
“Vijana hawa wanaohitimu sasa wameweza kupata chochote ambacho kitaisaidia jamii na kujisaidia wenyewe na pia kwenda kupunguza vile vitendo ambavyo vingeweza kuathiri jamii kwa kujiajiri.
“Nawapongeza nyie vijana, lakini nawaambia kuwa kuna fursa katika halmashauri zote nchini na kwa Halmashauri ya Temeke vijana wafahamu kuna mikopo ya asilimia 10,”ameeleza Chami.
Amebainisha kuwa asilimia 10 inayotolewa na halmashauri zote nchini kwa ajili ya kusaidia makundi maalumu, ambapo mkopo huo hauna riba unatolewa kwa vijana, watu wenye ulemavu na wanawake.
Chami amesema ili kupata mkopo huo vijana wanatakiwa kuwa watano kwenye kikundi, ambao ni watu walioungana kwa lengo moja.
“Vijana mliopata mafunzo hapa muunde kikundi na muwe na katiba inayowaongoza kunakuwa na masharti, kinapatikana wapi, waliopo wana sifa zipi na inatakiwa kusajiliwa ni bure.
Amefafanua kuwa kama kikundi kinataka kukopa kinaenda maendeleo ya jamii watampa njia ya kukopa wanatakiwa kutoka halmashauri moja au kama wanatoka zaidi ya moja wawe na barua inayowatambulisha mitaa waliyotoka.
“Andiko la mradi ni muhimu mtoe elimu kwa vijana wengine kuanzia miaka 18 hadi 35 na wa kike wakifikisha umri zaidi unaingia kwa kina mama nyie mnaohitimu muangalie ni kitu gani mnachoweza kufanya katika graphic design, ile elimu ikalete mafanikio katika jamii mkapeleke huduma,”amesisitiza.