Vijana watakiwa kujiepusha dawa za kulevya

MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele amewataka vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo bangi kwani itachangia kusitishwa mikataba yao.

Meja Jenerali Mabele ameyasema hayo wakati akihitimisha Mafunzo ya Awali ya Kijeshi kwa Vijana wa Kujitolea Operesheni Jenerali Venance Mabeyo katika kikosi cha Rwamkoma JKT mkoani Mara.

Advertisement

Amasema ni vyema kwa vijana hao ambao wamemaliza mafunzo ya awali ya kijeshi kutunza afya zao pamoja na kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo bangi kwani kosa hilo linaweza kuwafanya wakasitishia mikataba yao.

Meja Jenerali Mabele amewasisitiza vijana hao kuishi kiapo cha utii, uaminifu na uhodari na kuendeleza nidhamu waliofunzwa kwani kijana asiye nidhamu hastahili kupewa madaraka.

Aidha, Meja Jenerali Mabele ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliwezesha jeshi hilo kuendesha mafunzo ya vijana wa Kitanzania.

Naye Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU), Kanali Makame Daima amewapongeza Vijana hao kwa kuitimu mafunzo yao na kuwataka kwenda kukiishi kiapo chao

Akimkaribisha Mkuu wa JKT kutoa nasaha na kufunga mafunzo hayo, Mkuu wa Tawi la Mafunzo JKT Kanali Aisha Matanza amesema vijana hao wamewawakilisha vijana wenzao katika makambi yote yaliyoendesha mafunzo hayo.

Akitoa taarifa ya Mafunzo, Kamanda Kikosi cha Rwamkoma JKT, Luteni Kanali Gaudencia Mapunda amesema, mafunzo ya vijana ya  Kujitolea Operesheni Jenerali Venance Mabeyo yalifunguliwa Novemba 28, 2022 katika Makambi ya JKT  na kuhendeshwa kwa majuma 16

Mafunzo hayo yalianza kuhitimishwa kwa nyakati tofauti kuanzia Machi 7, 2023 hadi leo hii Machi 17, 2023 Mkuu wa JKT amefunga zoezi la uhitimishwaji wa mafunzo hayo.