Vijiji Newala kunufaika ujenzi zahanati

ZAIDI ya wakazi 6,000 wa vijiji mbalimbali katika Halmashauri ya Mji wa Newala mkoani Mtwara watanufaika na ujenzi wa zahanati iliyojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF) kwa gharama ya Sh milioni 100.

Kukamilika kwa zahanati hiyo kuwaondelea adha ya kutembea umbali takribani kilometa 8 kufata huduma za afya.

Advertisement

Akizungumza Julai 18, 2023 katika mkutano wa hadhara uliyofanyika kijiji cha Msilili kata ya Mtumachi uliyoandaliwa na mbunge wa jimbo la Newala Mjini ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu (Kazi Maalum), George Mkuchika, Mwenyekiti wa kijiji hicho Abdulaziz Michapacha ameupongeza mfuko huo na serikali kwa ujumla kwa kusikia kilio chao .

‘’Kilio cha zahati kwa wakazi wa maeneo haya ni cha muda mrefu huduma tulikuwa tunaipata kijiji jirani ukipata tatizo la usiku inakuwa mtihani na sisi tulikuwa na wazo hili kwa muda mrefu lakini hatukuwa na uwezo wa kujenga ilipofika serikali ikafanya maamuzi haya kwakweli tunashukuru sana na mradi utaenda kunufaisha wananchi hiki cha hiki na vijiji jirani kama vile Mitumbati, Chikwedu vyote viko kwenye kata hii .”amesema Michapacha.

Amesema wananchi wa kijiji hicho wanakabaliwa na adha kubwa ya upatikanaji wa huduma hiyo hivyo kulazimika kwenda kijiji jirani cha Tawala kufata matibabu ila walikaa chini kujadili namna wanavyoweza kupata huduma hiyo.

Mkazi wa kijiji cha Msilili kwenye halmashauri hiyo, Zaituni Mussa amesema: ‘’Zahanati hii itatupunguzia usumbufu mkubwa tunaoupata sasa katika huduma hii, huduma tunapata kijiji jirani cha Tawala pana urefu kidogo kutoka hapa kwahiyo imeturahisishia tuna uhakika wa kupata huduma karibu muda wote mtu anapopata tatizo mfano sisi akina mama hasa wakati wa kujifungua kwahiyo tunaishukuru Tasaf na serikali yetu kusikia kilio chetu.”

Ofisa Ufatiliaji wa Tasaf Wilaya ya Newala, Emmanuel Luhanzo amesema wameguswa kujenga zahanati hiyo kutokana na uhitaji mkubwa uliyopo kwa wakazi wa maeneo hayo ambao wanatembea umbali huo mrefu kwenda kijiji jirani kufata huduma hiyo.

Amesema mchakato wa ujenzi huo ulikuwa ni wazo kutoka kwa wananchi hao ambalo waliliibua mwaka 2022 kuomba wajengewe zahanati kupitia mfuko huo kwakuwa ni moja ya hitaji lao na katika gharama hiyo ya ujenzi asilimia 90 ya mradi wote umefadhiliwa na Tasaf asilimia nyingine 10 mchango wa jamii.

Naye mbunge wa jimbo hilo, ameupongeza mfuko huo kwa kuchagua halmashauri hiyo kujenga zahanati kati ya halmashauri 184 zilizopo nchini ikiwemo Newala ujenzi ambao utaendelezwa na matundu sita ya vyoo ikiwemo matatu upande wa wanawake mengine matatu wanaume na suala la vichomea taka.

Amesema kazi iliyobaki upande wa halmashauri ni kuhusu vifaa tiba pamoja na watumishi na serikali kwa mwaka wa fedha uliyopita imeleta fedha kwa ajili ya kujenga vituo viwili vya afya kwenye halmashauri hiyo ikiwemo Kijiji cha Nambunga na Nanguruwe.

Mbungu huyo katika ziara yake hiyo inayoendelea jimboni humo amefanikiwa kuzungumza na wananchi kwenye vijiji mbalimbali katika halmashauri hiyo ikiwemo Chikwaya, Mcholi godauni na Tumaini, Msilili na Mitumbati, Chiunjila, Chihanga pamoja na Mapili.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *