KIASI cha Sh bilioni 14 za biashara ya hewa ukaa zilizotolewa hivi karibuni kwa vijiji vinane vya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi zimeongeza chachu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kuhifadhi misitu yake ili nayo inufaike na biashara hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ni moja kati ya halmashauri saba nchini ambazo kwa kupitia kata 18 na vijiji vyake 54 zinatekeleza Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) nchini.
Mbali na Halmashauri ya Tanganyika na Iringa zingine zinazonufaika na mradi huo ni pamoja na halmashauri ya wilaya ya Mbeya na Mbarali (Mbeya), Halmashauri ya Sumbawanga Vijijini (Rukwa) pamoja na halmashauri za wilaya ya Tanganyika na Mpimbwe (Katavi).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Selemani Jafo pamoja na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Maji na Mazingira ikiongozwa na mwenyekiti wake Mbunge wa Kalenga Jackson Kiswaga imetembelea kata ya Nzihi wilayani Iringa ambayo ni moja ya kata hizo 18 zinazotekeleza mradi huo.
Katika kata hiyo kamati hiyo imejionea miradi inayotekelezwa kupitia SLR ikiwa ni pamoja na hifadhi ya misitu katika kijiji cha Ilalasimba na Magubike, shamba darasa la kilimo cha mazao, shamba darasa la malisho ya mifugo, na mradi wa ufugaji wa Ng’ombe wa maziwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Swaum Kweka alisema katika kata hiyo jumla ya hekta 9500 zimehifadhiwa na kuleta mabadiliko chanya katika jamii ikiwa ni pamoja na kupungua kwa shughuli za ukataji miti, uchomaji mkaa na kurejea kwa vyanzo vya maji ambavyo vimeanza kutiririsha maji.
“Tumeona miradi hii ya uhifadhi wa mazingira jinsi inavyosaidia kulinda bioanuai, kupunguza uharibifu wa ardhi, kulinda vyanzo vya maji, kupunguza mabadiliko ya hali ya hewa, kupunguza umasikini na kupunguza uchafuzi wa hewa,” alisema Waziri Jafo.
Jafo alisema miradi ya uhifadhi wa mazingira inaweza kuchangia katika kupunguza mabadiliko ya hali ya hewa kwa kufyonza hewa ukaa kutoka kwenye anga kupitia msitu na akatangaza mpango wa wizara yake unaolenga kuviunganisha vijiji vyote vya mradi wa SLR na biashara ya hewa ukaa.
Mratibu wa kitaifa wa SLR, Dk Damas Mapunda alisema Mradi wa SLR unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kwa zaidi ya Sh Bilioni 25.8.
Alisema mradi huo unalenga kurejesha uoto wa asili na kuhifadhi mazingira huku ukiangalia namna ya kuwawezesha wananchi kufanya shughuli mbadala za kiuchumi kama ufugaji na kilimo ili wajiepushe na uharibifu wa mazingira.
Mbali na ufugaji na kilimo, Dk Mapunda alisema katika mipango yake, mradi huo umekusudia kuvihamasisha vijiji vyote vya mradi kuingia katika biashara ya hewa ukaa.
“Vijiji nane vya halmashauri ya wilaya ya Tanganyika vilivyopo katika mradi huu vina zaidi ya hekta 100,000 za misitu ya hifadhi. Vimekamilisha taratibu za kuingia kwenye biashara ya hewa ukaa na vitakuwa vikipata fedha za biashara hiyo mara mbili kila mwaka, mwezi Juni na Desemba,” alisema.
Alisema hivikaribuni vijiji hivyo vimepokea Sh Bilioni 14, mgao wa Desemba mwaka jana ambazo kati yake asilimia 20 zinakwenda katika halmshauri ya wilaya hiyo, huku sekretarieti ya mkoa nayo ikiomba asilimia moja.
“Mapato haya ni makubwa sana kwa vijiji nane. Yamewawezesha kuwakatia bima ya afya wananchi wake wote lakini pia yataviwezesha vijiji hivyo kujenga vyenyewe sehemu kubwa ya miradi yao ya afya, barabara, elimu, maji na mingineyo,” alisema.
Dk Mapunda alisema mpango wao wa hivikaribuni ni kuziwezesha kamati za mazingira za halmashauri sita kwenda katika halmashauri hiyo ya Tanganyika ili waweze kujifunza namna wenzao walivyofanikiwa kuingia katika biashara hiyo.
Akizungumzia uwezekano wa kata ya Nzihi kuingia katika biashara hiyo, Dk Mapunda alisema wanahitaji kuvishawishi vijiji jirani na kata hiyo viingie katika mpango huo ambao moja ya masharti yake ni kuwa na msitu unaoanzia ukubwa wa hekta 25,000.
“Kata ya Nzihi ina misitu yenye ukubwa wa hekta 9,500, kwahiyo ili wawe na hekta 25,000 ni lazima watafute vijiji vya kufanya navyo ubia nje ya kata yao,” alisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Kiswaga kwa upande wake alisema wananchi wanaojitolea katika kutunza mazingira wanachangia kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha kwamba mazingira yanayostawi leo yanabaki kuwa salama na yanayoweza kusaidia vizazi vijavyo.
“Tunamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele mipango inayohamasisha utunzaji wa mazingira nchini. Mipango hii inalenga kukinusuru kizazi hiki na kijacho,” alisema.